TETESI ZA USAJILI BONGO: Yanga kurudi kwa Yacouba Songne, Kagere bado yupo sana

KLABU ya Yanga huenda ikamsajili tena aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Burkina Faso, Yacouba Songne kwa ajili ya msimu ujao.

Nyota huyo aliyejiunga kwa mara ya kwanza na Yanga mwaka 2020 akitokea Asante Kotoko ya Ghana, huenda akajiunga na timu hiyo huku akiwahi kucheza klabu mbalimbali zikiwemo Ihefu na AS Arta Solar7.

NAMUNGO imeonyesha nia ya kumsajili moja kwa moja mshambuliaji wa kikosi hicho, Meddie Kagere. Nyota huyo aliyewahi kutamba na Gor Mahia na Simba, alijiunga na Namungo kwa mkopo akitokea Singida FG na sasa wanataka kumbakisha jumla, japo anasikiliziwa ataamua nini.

SINGIDA Black Stars, imeanza mazungumzo ya kumnasa beki wa kati Mcongomani, John Nekadio kutoa RFC Seraing ya Ubelgiji.

Hata hivyo, inaelezwa viongozi wa RFC Seraing upo tayari kumtoa kwa mkopo na sio kumuuza moja kwa moja hivyo kuwataka Singida kulipa Dola 100,000 kuipata saini ya beki huyo wa kati.

KIPA chipukizi wa Simba, Ahmed Feruzi inadaiwa atatolewa kwa mkopo kati ya Kagera Sugar au KMC, lengo ni kuhakikisha anapata muda wa kucheza na uzoefu.

Imekuwa ngumu kwa Feruzi kupata nafasi ya kucheza mbele ya makipa waliopo Simba, Ayoub Lakred, Ally Salim na Hussein Abel ambao angalau wanapata nafasi ya kucheza.

UONGOZI wa Mbeya City iliyopo Ligi ya Championship, upo katika mazungumzo ya kumpatia mkataba mpya mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Eliud Ambokile.

Hata hivyo, inaelezwa Ambokile aliyewika na klabu kama Nkana, TP Mazembe na Black Leopards, shauku yake kubwa ni kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao hivyo ni ngumu kusalia Mbeya City.

TANZANIA Prisons, wamedaiwa kuwasiliana na kipa wa Geita Gold, Samson Sebusebu ili kujiunga na timu hiyo msimu ujao. Viongozi wa Prisons wanamuona Sebusebu kama mbadala sahihi wa kipa namba moja wa timu hiyo, Yona Amos iwapo ataondoka akiwindwa na klabu zaYanga, Fountain Gate na Namungo.

KLABU ya Coastal Union imeingilia dili la nyota wa Geita Gold, Edmund John ambaye mkataba wake na kikosi hicho umeisha rasmi. Coastal itakavyoshiriki na michuano ya kimataifa, imeanza kuvutiwa na huduma ya winga huyo aliyeanza kuwasiloiana na Mashujaa inayomhitaji, huku Pamba Jiji ikitajwa kujitosa kumuwania.

Related Posts