Mkongo wa baharini wa Airtei 2Afrika kuanza kutumika rasmi

Dar es Salaam. Airtel Tanzania imeanza kutumia rasmi Mkongo wa mawasiliano unaopita baharini wa 2Africa wenye urefu wa kilomita 45,000 ukiunganisha mabara matatu ili kutoa huduma za intaneti ya kasi zaidi, jambo litakaloleta maendeleo makubwa katika kupanua na kuimarisha miundombinu ya kidijitali nchini Tanzania.

Mkongo huu wa kisasa wa 2Africa unaopita chini ya Bahari na kusimamiwa na Airtel Tanzania unatarajiwa kuiweka Tanzania katika viwango vya juu   vya mabadiliko ya kukua kwa huduma za kidijitali, na kukidhi mahitaji ya uchumi wa nchi unaoendeshwa na huduma za mtandao (data).

Mkongo huo umezinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kituo cha Mkongo wa mawasiliano baharini – Airtel Cable Landing Station kinachotua Dar es Salaam maeneo ya Mbezi beach. Pia alizindua mtandao wa 5G wa Airtel Tanzania tukio lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.

Amesema mkongo huo utaleta mabadiliko chanya ndani ya sekta ya mawasiliano katika kuboresha uchumi wa Tanzania kupitia huduma bora kidijitali.

“Kuzindua Kituo cha 2Africa Cable landing Station kunaashiria hatua muhimu na mustakabali wa nchi yetu kupaa kidijitali. Miundombinu hii sio tu italeta mapinduzi katika huduma za mawasiliano pia itaharakisha ukuaji wa uchumi kwa kuimarisha muungano na mataifa mengine,” amesema Rais Samia

Mkongo wa 2Africa sasa umeanza rasmi kuhudumia makampuni ya teknolojia ambayo sasa yanapokea masafa ya uwezo wanaohitaji kupitia kituo cha Airtel Cable Landing Station   kilichopo Dar Es Salaam Mbezi Beach

Mkongo mpya wa Airtel 2Africa unatarajia kuwa suluhisho na ulinzi wa mikongo au kebo zingine za mawasiliano zinazopita chini ya bahari nchini. Uzinduzi huu wa Airtel Tanzania umekuja kutokana na kukatika kwa nyaya za mkongo wa mawasiliano unaopita chini ya bahari hivi karibuni ambazo ziliathiri baadhi ya maeneo ya Afrika Mashariki, ikiwemo  Tanzania.

Mkongo wa mawasiliano wa 2Africa unauwezo wa kusafirisha masafa mara 10 zaidi ya ile iliyopo na inalenga kusaidia kuanzishwa kwa vituo vya kuhifadhi kumbukumbu kieletroniki (Data centres)  ili kukidhi ongezeko la shughuli za kidijitali nchini.

Kuwashwa kwa Mkongo wa   2Africa kutaleta manufaa makubwa katika kuikuza Tanzania ya ya kidijitali kutokana na kuboreshwa kwa matumizi ya mtandao katika uhamishaji wa maudhui na kuhakikisha kasi ya juu ya 4G na 5G kwa watumiaji. Mkongo wa mawasiliano wa 2Afrika inaiunganisha Tanzania na maeneo 43 duniani, na inahudumia zaidi ya watu bilioni 3 na kukuza muunganiko wa kimataifa wa wafanyabiashara kidijitali. Mkongo huu unaunga mkono mipango ya Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, ikiwemo mipango ya maabara ya akili mnemba na maabara za roboti.

Mkurugenzi Mkuu wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh, amesema kwamba mazingira wezeshi ya serikali katika kupatikana kwa leseni pamoja na uwepo wa mfumo bora wa udhibiti ndio sababu zilizowezesha Airtel Tanzania kuzindua kituo chao cha Airtel 2Africa kabla ya nchi nyingine. Alieleza kuwa Tanzania inashuhudia kuwashwa kwa mkongo wa 2Africa na kuanza kugawa masafa yenye uwezo wa juu moja kwa moja sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari amesema kuwa Mkongo huu mpya wa mawasiliano unaopita baharini utachochea na kuboresha zaidi huduma bora za intaneti nchini.

“Mkongo huu mpya utakuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na mahitaji ya huduma za mtandao wa intaneti nchini, ambapo mahitaji yake yamekuwa yakioongezeka maradufu kila baada ya miaka miwili. Nina hakika kuwa teknolojia hii itapelekea utekelezaji wa haraka wa mkakati wetu wa kuhimiza matumizi ya TEHAMA katika sekta zote na kuboresha uchumi wa kidijitali ambao Tanzania inatamani kufikia,” alisema Dk Bakari.

Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema uwepo wa Mkongo wa huo utasaidia kuunganisha nchi kimataifa na kuwepo kwa mifumo ya kibunifu kidijitali ikiwemo kuunganisha mifumo mbalimbali ya serikali kuwa jumuishi.

“Mkongo wa 2Africa utaleta maendeleo kwa huduma za mawasiliano katika nchi yetu na kuwa kivutio na suluhisho la mawasiliano kidigitali kwa nchi za Afrika Mashariki,” amesema Nape

Kulingana na makadirio ya RTI International, Mkongo wa 2Africa unatarajiwa kuzalisha kati ya USD 26.4 bilioni na USD 36.9 bilioni ikiwa ni matokeo ya ukuaji kiuchumi kutokana na huduma zitakazotolewa na mkongo huu barani Afrika ndani ya miaka ya awali.

Related Posts