Kocha: Kuna balaa Taifa Cup

BAADA ya timu ya kikapu ya Mkoa wa Kigoma kuifunga Morogoro kwa pointi 106-54 katika mashindano ya kombe la taifa, kocha wa timu hiyo, Qassim Anasi amesema licha ya kushinda amekiri ushindani ni mkubwa mwaka huu.

Mashindano hayo mwaka huu yanafanyika katika viwanja Chinangali mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo na Mwanaspoti kwa simu, Anasi alisema ushindani unatokana na uwezo mkubwa wa wachezaji walionao kwa timu zote shiriki kutoka katika mikoa tofauti.

Alisema ubora wa timu hizo unatokana na mikoa mingi kufanya usajili wa wachezaji nyota wanaocheza katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL).

“Timu zilipewa nafasi na TBF (Shirikisho la Kikapu Tanzania) kusajili wachezaji wasiozidi watano kutoka nje ya mikoa yao na mikoa hiyo ilitumia nafasi hiyo ya kuchukua wachezaji nyota kutoka Dar es Salaam,” alisema Anasi.

Hata hivyo kocha huyo alizitaja baadhi ya timu zitakazotoa upinzani kwa timu yake kuwa ni pamoja Mtwara, Manyara, Dodoma na Unguja.

Akiizungumzia Dodoma, alisema licha ya kuifunga katika mchezo wa kwanza kwa pointi 49-42, timu hiyo ina uwezo mkubwa na mbinu za kisasa za uchezaji.

Akizungumzia ushindani, nyota wa Kigoma, Amin Mkosa  alisema kwa upande wa wachezaji wamejipanga kupambana  vilivyo ili kushinda michezo yote iliyo mbele yao.

Related Posts