Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema wapiga kura 594,494 wataondolewa katika daftari la kudumu la wapigakura kwa kupoteza sifa.
Wapigakura hao wamepoteza sifa kutokana na kufariki dunia, hayo yakiwa ni makadirio ya tume kupitia Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Idadi hiyo itaondolewa wakati tayari tume imetangaza kusogezwa mbele uboreshaji wa daftari Ia kudumu Ia wapigakura hadi Julai 20, 2024 badala ya Julai mosi, 2024 iliyopangwa awali.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Juni 24, 2024 na mkurugenzi wa idara ya habari na elimu ya mpigakura wa INEC, Giveness Aswile alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.
“Takwimu hiyo ya wasio na sifa ni makadirio ya waliofariki dunia kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022,”amesema.
Aswile amesema vitu vingine vinavyomfanya mtu apoteze sifa ni kufungwa kwa zaidi ya miezi sita gerezani, kutokuwa na akili timamu pamoja na kukiuka sheria za uchaguzi.
Tume hiyo imeeleza kuwa wapigakura 4,369,531 wataboresha taarifa zao.
Idadi hiyo ya wapigakura wanaotegemewa kuboresha taarifa zao ni wale ambao taarifa zao zilikosewa au wamehama kutoka kata au jimbo moja kwenda eneo lingine la uchaguzi na wengine ni wale ambao kadi zao zimeharibika au zimepotea.
Kwa mujibu wa tume hiyo, kwa kutumia ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya Sensa ya Watu na Makazi, idadi ya wapigakura itaongezeka hadi kufikia milioni 34.7 kutoka milioni 29.75 ya wapigakura wa mwaka 2020.
Idadi hiyo itajumuisha wapigakura wapya milioni 5.58 ambao ni sawa na asilimia 18.7 wanaotarajiwa kuandikishwa.