Wadau waitwa kuwekeza sekta ya mifugo Tanzania

Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewaita wadau kuwekeza katika sekta za malisho, chanjo, maji ya mifugo na majosho, ili kuleta matokeo chanya katika sekta hiyo.

Ulega ametoa wito huo leo Jumatatu Juni 24, 2024 katika uzinduzi wa taarifa ya 21 ya uchumi wa Tanzania iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB), yenye kichwa cha habari ‘Kutumia fursa ya kuwa na sekta ya ufugaji inayokabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na yenye ushindani Tanzania.’

Amesema taarifa ya benki hiyo imeeleza kwa undani kupitia utafiti uliofanyika, ikionyesha kuna fursa kubwa katika sekta ya mifugo, licha kuwepo kwa changamoto mbalimbali.

Mbali na hilo, amesema kunahitaji uwekezaji zaidi wa pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi, ili sekta ya mifugo izidi kusonga mbele.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya Benki ya Dunia imetaja maeneo yanayotakiwa kuboreshwa, ili kuleta matokeo bora katika sekta ya mifugo ambayo ni udhibiti wa magonjwa, huku Serikali ikijipanga kwa kutenga bajeti ya Sh28 bilioni.

“Jambo jingine ni sekta ya maji ambayo tunashirikiana na Wizara ya Maji, lakini pia suala la malisho limeonekana linahitaji uwekezaji zaidi kutoka kwa wadau, ili mifugo kupata nyasi za uhakika zitakazonenepesha mifugo yao kwa wakati.

“Pia kunahitajika mbegu za mifugo zenyewe, ili tuwe na mifugo bora ikilinganishwa na hiki tulicho sasa,” amesema Ulega.

Kwa upande wa chanjo, amesema kuna kazi kubwa ya kufanya, akisema Serikali imeingia katika mkakati utakaohakikisha mifugo yote inapata chanjo, ili kuzuia maradhi yanayoenea kwa mifugo.

Waziri Ulega amewaomba wadau wa mifugo, kuendelea kutoa ushirikiano katika sekta hiyo, akisema suala la mifugo ni la kila mtu na Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wote, wakiwamo wafugaji na wawekezaji.

“Upande wa Serikali tumeshafanya ndani ya miaka mitatu, tumetoka katika kiwango cha Sh31 bilioni hadi Sh112 bilioni, mafanikio mazuri yanayonyesha mwanga mkubwa mbele ya safari katika sekta ya mifugo, lakini tunahimiza sekta binafsi kufanya uwekezaji zaidi,” amesema.

Hata hivyo, taarifa ya Benki ya Dunia imeonyesha uwekezaji katika sekta ya mifugo bado mdogo ukilinganisha na fursa zilizopo katika sekta hiyo. Licha ya kuipongeza Serikali kwa jitihada zinazochukuliwa za kukuza sekta ya mifugo, imesema kuna haja ya kuongeza nguvu zaidi.

Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia-Tanzania, Nathan Beleta amesema Tanzania ni Taifa lenye idadi ya mifugo inayokua kwa kasi katika bara la Afrika na duniani.

Amesema kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na ng’ombe milioni 36.6 na kuifanya kuwa ya pili kwa idadi kubwa barani Afrika, baada ya Ethiopia.

Hata hivyo, Belete amesema  kulingana na ripoti zilizopo, sekta ya ufugaji na malisho, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kunyesha kwa mvua na joto kali.

“Magonjwa ya mifugo yanayoenea yanaathiri afya ya wanyama, tija na upatikanaji wa soko,” amesema Belete.

Related Posts