Dodoma. Mjadala wa sukari umeendelea kulitikisa Bunge huku Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara akisema kama wapo mawaziri au wabunge wanaodaiwa kupewa rushwa katika suala hilo watajwe bungeni ili washughulikiwe.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Serikali leo Jumatatu Juni 24 2024, Waitara amesema suala hilo limekuwa likiwachanganya.
“Na kama kuna waziri ama mbunge amekula rushwa hawa watu watajwe hapa washughulikiwe, tusichafuane humu ndani hili jambo naomba mheshimiwa Rais (Rais Samia Suluhu Hassan) na wewe spika mlishughulikie tujue ukweli ni upi tuweze kuamua,” amesema.
Mwita amesema hilo ni Bunge la Watanzania linaloonyeshwa moja kwa moja na kuhoji iweje itajwe rushwa kwenye suala hilo.
“Kuna waziri ameleta mpango hapa, lakini mnasema kuna waziri mwenzie amemhujumu, hawa wanamhujumu mheshimiwa Rais, ikitokea la kutokea humu ndani, wote tutalaumiwa hatuwezi kutoka kwa hiyo jambo la sukari lishughulikiwe. Tuitwe kama semina iwe open (ya wazi) discussion (mjadala wa wazi),” amesema.
Ametaka wabunge kuelezwa faida ya kuingiza sukari kutoka nje ya nchi ni ipi na ya kuimarisha viwanda vya ndani ni ipi, kusudi waweze kuamua kama Watanzania badala ya kuamuliwa na baadhi ya watu ambao watawalisha matango pori.
“Hili ni jambo muhimu sana, lisifanyiwe kampeni kama kuna watu walienda katika korido watajwe na hawa hawafai kuendelea kuwa wabunge kwenye Bunge hili kwa sababu hawana uzalendo wowote,” amesema Waitara.
Mbunge wa Nzega Vijijini (CCM), Dk Hamis Kigwangalla amesema jambo analolifanya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe katika kudhibiti bei ya sukari, hauwezi kutarajia kuwa uamuzi wa namna hiyo unaungwa mkono na watu wanaonufaika na kukosekana kwa bidhaa hiyo.
“Pengine wana mawazo kuwa huenda biashara yao ikaathirika pengine ndio inaleta vuguvugu hili ambayo wanakumbana nayo Waziri Bashe na Serikali kwa jumla katika kipindi hiki.
“Hoja za aina hii huwa zina msukumo wa wafanyabiashara wakubwa wanaofaidika na mfumo kandamizi kwa walaji wa mwisho, hata wanaotoa hoja kwamba uwepo wa mfuko huu utaathiri viwanda vya ndani labda hawajafanya tafakuri ya kina,” amesema.
Amesema anachofanya waziri ni kutengeneza mfumo wa kuwalinda walaji huku akiwataka wanasiasa kuunga mkono suala hilo kwakuwa anaenda kulinda wananchi wa hali ya chini.
Naye Mbunge wa viti maalumu (CCM), Lucy Mayenga amependekeza wafanyabiashara wenye uzalendo wapewe kipaumbele kwenye utaratibu wa ziara za Rais Samia Suluhu Hassan.
“Haiwezekani ukawa wewe umekaa na kampuni yako inafanya hujuma kwenye sukari, huku tunakuona upo kwenye ziara ya Rais, inauma sana mtu amekaa kwenye runinga unamuona na mfanyabiashara fulani yule halafu huku ndiye mtu anayeshughulika sukari isipatikane,” amesema.
Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM) Dk Pius Chaya amesema kama kuna watu wanaohujumu sekta ya sukari ni muda muafaka kwa Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria.
“Mheshimiwa Mwigulu (Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba) na Mheshimiwa Bashe wekeni sheria kali ikitokea kuna upungufu wa sukari kuna mtu anaficha sukari wekeni sheria kali kumfungia kabisa ama vitu vingine,” amesema.
Naye Mbunge wa Igalula (CCM), Venant Protas ameunga mkono pendekezo la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kupewa mamlaka ya kuagiza bidhaa hiyo kama ilivyoidhinishwa katika hotuba ya bajeti kuu ya Serikali.
“Sukari ni suala la masilahi ya nchi, tuwatetee wananchi badala ya kuingiza siasa, kwenye mambo ya siasa ndio tuwe na siasa, ” amesema.
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Mariam Ditopile amesema Bunge ndio lilipitisha sheria kwa nia njema ya kutoa vibali kwa wazalishaji wa sukari kwa maana ya viwanda ili waingize bidhaa hiyo nchini kunapokuwa na uhaba.
“Sheria tunatunga zinaenda kutungiwa kanuni ili zifanye kazi, kwa hiyo sio dhambi kukaa, kujitathimini na kujisahihisha kama sheria imeleta matatizo kwa wananchi sio dhambi, mabadiliko ya sheria ya sukari yaungwe mkono maana nia ni njema ya kusaidia wananchi,” amesema.