HADITHI: Zindiko (sehemu ya 3)

DIWANI akatabasamu kidogo, kisha akafuta tabasamu lake alipoanza kuzungumza.

Bwana Zimataa. Unaikumbuka ahadi yangu wakati wa kampeni za uchaguzi wa hapa kwetu?

Alikumbuka kila alichokuwa akikizungumza wakati wa kampeni kinachoendana na ndoto zake kuhusu eneo hilo. Alipokuwa akinadi sera zake, alikuwa haadhi kuzungumzia jengo la Zindiko. Na alikuwa akiongea mambo ambayo hayajui. Lakini aliongea kwa ujasiri mkubwa kiasi kwamba watu wakatamani kuona utekelezaji wake – ndio maana wakamchagua.

Lakini Mzee Zimataa alitaka aseme mwenyewe. Kwa hiyo akanyamaza na kumwacha aendelee kuzungumza

“Kama umesahau nitakukumbusha. Nilikula kiapo kumaliza tatizo la jengo lenu hili lenye zindiko tishio kwa maisha ya watu wa hapa. Kwamba kama jengo hili litaendelea kuwepo, basi wananchi wawe huru kufika hapa bila kuhofia maisha yao… au vinginevyo nguvu ya aina yoyote, iwe ya nguvu za giza au nguvu za serikali zitumike kulivunja lisiwepo tena.”

Mzee Zimataa akamtazama tu. Kwa sababu alichokuwa akikizungumza, kilikuwa kama wimbo wa kumtishia nyau mtu mzima.

“Kwamba katika eneo langu, haiwezekani kuwa na jengo ambalo watu wanakufa kwa kumezwa na joka pale wanapothubutu kuingia kwenye viunga vyake, hata kwa bahati mbaya tu.”

Akatangulia kukataa kwa ishara ya kichwa kuweka msisitizo kwenye sentensi yake inayofuata. “Hiyo sio katika utawala wangu. Hizi ni zama za mwisho kwa Joka la Zindiko.”

Mzee Zimataa akaendelea kumtazama shujaa na jasiri huyu akiendelea kumthibitishia Mbunge kuhusu ujasiri wake wa kuzungumza.

“Nimeshakuhoji mara kadhaa kwamba ni nani mmiliki wa jengo hili, lakini hutoi ushirikiano. Wananchi wameanza kuuulizia hiyo ahadi yangu, maana ni miezi sita ishapita tangu nichaguliwe. Kwa hiyo nipo katika mkakati wa kutimiza ahadi yangu kwa jengo hili.

Ikawa ni zamu ya Mzee Zimataa kujibu. Kwanza akageuka nyuma kuliangalia jengo analolisimamia. Kissha akaelekeza uso kwao.

“Sawa, nimekusikiliza vizuri. Na unajua kwamba hii si mara ya kwanza kusikia kauli zako hizi. Lakini naona leo umetamka kwa ujasiri zaidi, pengine kwa sababu upo na Mheshimiwa Mbunge na umemuahidi hayohayo uliyowaahidi wananchi. Lakini inavyoonekana wewe hunifahamu mimi vizuri.

“Leo nitakwambia kile ambacho kipo. Nitakupa majibu ambayo unastahili kuyapata tena kwa mara ya mwisho, maana sitakuja kurudia tena.

“Kitu cha kwanza ambacho unatakiwa kujua ni kwamba uchokifanya ni kupima maji ya mafuriko kwa kutumbukiza miguu yenu.”

Diwani akamtazama bila kuitikia.

“Labda kwa niaba ya Mbunge wako, nijitambulishe upya na rasmi kwako. Mimi naitwa Zimataa. Hili jina sikupewa kwa bahati mbaya. Nilifika kijijini hapa miaka 22 iliyopita na nikanunua ardhi, nikajenga nyumba yangu kule ninakoishi hivi sasa!

“Jengo hili unaloliona hapa lilijengwa nikiwa niko hapahapa na mafundi waliotoka mjini. Sikushiriki kwa namna yoyote na wala mmiliki wake sikumuona. Licha ya uimara wake mnaouona nao, lakini jengo hili limejengwa kwa muda mfupi sana. Nahisi sasa kuna haja ya kukusimulia – vumilia ujue undani wangu na wa hapa, labda itakusaidia.”

Mbunge na Diwani wakamtumbulia macho kumsikiliza. Mzee Zimataa akaanza kumsimulia.

“Wakati linajengwa, nilikuwa nikipita tu njia na kuendelea na hamsini zangu. Kutokana na jengo lenyewe kujengwa katikati ya pori kubwa – maana hapa zamani palikuwa ni msituni – nilichukulia kwamba hiki lazima kitakuwa kiwanda cha mwekezaji kutoka mjini.

“Siku moja nilipopita upande huu, nikaliona likiwa limekamilika.

“Lilikuwa ni jengo zuri sana, linalopendeza na kuvutia macho ya yeyote. Yaani utafikiri lilikuwa limeshushwa kutoka mbinguni. Mazingira yote haya yalikuwa maridadi. Maua yalioteshwa pande zote hizi na kulifanya lipendeze kama ikulu.

“Si unaliona lilivyo kubwa na imara? Lilijengwa kwa miezi mitatu tu – kisha kila kitu kikawa kimekwisha.

“Kisha siku moja isiyo na jina, Mwanaume mmoja mtu mzima alisimama katikati ya uwanja wa jengo hili akiwa amevaa shuka jeusi na shanga za rangi kadhaa zilizofungwa kichwani na barakoa nyeusi. Alishika fimbo kubwa. Mbele yake kukawa na watu wenye mashuka na barakoa nyeusi wameinamia chini kwa adabu.

“Huyu alikuwa ni mtu kutoka nchi za mbali. Na hao walikuwa ni wasaidizi wake. Walikuwa wafanya tambiko kubwa la jengo hili. Walikuwa wanaweka zindiko. Inawezekana hili likawa ni tambiko kubwa na zito kuliko yote duniani. Na lilifanyika kwa siku tatu.

“Unajua maana ya zindiko? Ni kinga ya nyumba au jengo lolote. Kwamba wabaya au mtu yoyote mwenye nia mbaya akisogea ataingia kwenye shida na maisha yake.”

Mzee Zimataa akaweka nukta ili kujiridhisha kwamba kile anachokizungumza kimeingia vizuri! Alikuwa anawapa ‘dawa’ kwamba iingie na ifanye kazi. Alipoona wako kimya, akaendelea.

“Sasa nakutamkia mwenyewe, kwamba hapa kuna joka lililoshindikana linalolinda jengo hili. Joka lililotokana na zindiko la nguvu za jiwe jekundu.”

Mbunge akaonekana kupata shauku nyingine, “Jiwe jekundu? Ndio jiwe gani hilo?”

Mzee Zimataa akatabasamu.

“Afadhali Mheshimiwa umeuliza swali ambalo huyu diwani yako hajawahi kuniuliza hata siku moja. Na ndiyo maana anajaribu kupambana. Kiufupi anapambana na kitu asichokijua.

“Jiwe jekundu, ni jiwe lililotokana na mwamba mmoja mkubwa uliokuwa kwenye mapango katika zama za kale za nchi za mashariki ya kati. Kwa ramani za dunia ya leo, inaaminika mwamba huo ulikuwa nchini Misri.

“Mwamba huo ulikuwa umegawanyika kwenye rangi tatu. Rangi nyekundu, Bluu na njano. Kila rangi hapo iliwakilisha aina ya madini yenye rangi tatu tofauti. Lakini kila moja ikiwa na nguvu zake za asili za kufanya chochote kwenye ulimwengu.

“Sitazama sana ndani kuhusu mawe hayo yote, lakini nataka kuwaambia kwamba mawe hayo yamepigwa marufuku kutumika duniani kote. Ni mawe yaliyokuwa na nguvu kubwa zilizopitiliza kwenye kila jambo na kwa kila jiwe. Yaani ni kama yaligawana kazi.

“Wengine walitengenezea vidani, wengine pete na wengine waliyatumia yenyewe kama yenyewe. Kimsingi watu walitumia nguvu za mawe hayo vibaya na kusababisha mabalaa makubwa kutokea duniani. Kwa hiyo yakapigwa marufuku.”

“Sasa mnajua mimi nilifikaje hapa? Na mnajua kwa nini nimekuwa mtu pekee mwenye mamlaka ya kuingia hapa na kutodhuriwa na hili joka na vyote vilivyomo kwenye tambiko hili? Nisikilizeni.

Baada ya tambiko hilo, mimi nilivutiwa na hapa. Na nilikuwa napita tu kwa mbali. Lakini kulikuwa na ajabu moja, licha ya uzuri wa jengo, lakini uzio wake ulikuwa mdogo na mfupi. Na la mwisho la kushangaza ni kwamba geti lake dogo, lilikuwa wazi muda wote.

Hii ikanipa tamaa ya kuingia ndani ya uzio na kwenda kuliona jengo hili kwa ukaribu zaidi. Kwa hiyo nilipolifikia jengo, nikavuka uzio na kuingia.

Nikasogea hadio katikati ya kiwanja, kwa hiyo nikawa ndani ya uzio, katikati ya uwanja wa mbele wa jengo.

Hapo nikagundua kitu. Nikagundua mbele ya jengo hili kwenye upande wake wa kulia, kuna mtungi wenye mdomo mpana. Kidogo ilinishangaza kwa sababu sikutegemea kwenye jengo la kisasa na kizungu kama lile, likawa na mtungi. Hili jambo kidogo likanishangaza na kunivutia zaidi kusogea na ikibidi kuchungulia ndani ya mtungi kwamba kuna nini.

Related Posts