JIRANI zetu Kenya wamekumbwa na maandamano makubwa yanayoongozwa na makundi ya vijana wanaopinga muswada wa sheria ya fedha uliowasilishwa bungeni na serikali inayoongozwa na Rais William Ruto.
Ukichambua kwa kina kinachoendelea nchini humo utaona pande zote mbili ziko sahihi kwa wanachofanya.
Wanaoandamana wanapinga muswada huo kwa sababu utakwenda kuathiri maisha moja kwa moja kwa kupandisha gharama za maisha. Wako sahihi kabisa.
Serikali nayo imepeleka muswada huo bungeni ili kupata fedha za kukabiliana na deni kutwa la taifa ambalo limelimbikizwa kwa miaka mingi.
Deni la taifa la nchi hiyo limefikia asilimia 70 ya pato la taifa ilhali maelekezo ya Benki ya Dunia yanataka deni la taifa la nchi lisizidi asilimia 55 ya pato la taifa.
Aprili 2023, serikali ya Kenya ilitangaza kwamba haikuwa na pesa za kulipa mishahara ya Machi mwaka huo kwa wafanyakazi wake.
Serikali ilikuwa imeishiwa kabisa na inaelekea kubaya. Ikabidi waende kukopa ili kupata pesa. Deni hilo na madeni ya nyuma yakaielemea serikali na kufikia hapa walipofika.
Kuna wakati ilizuka hofu kwamba serikali ya China itaichukua bandari ya Mombasa kama fidia ya deni la ujenzi wa reli ya SGR kutoka Nairobi hadi Mombasa ambalo serikali ya Uhuru Kenyatta ilikopa.
Japo baadaye ulitolewa ufafanuzi rasmi kwamba hiyo haikuwa ukweli, lakini waliozusha walipita na upepo wa madeni uliokuwa ukivuma Kenya kwa muda mrefu.
Kenya imefikia scheme ya kuwa haikopesheki tena na wanaodai wanadai kwelikweli…na serikali haina chanzo kingine cha mapato kilichobaki zaidi ya kuwageukia wananchi kupitia kodi…ndiyo huu muswada ambao wananchi wanaupinga.
Kinachoendelea Kenya kimetokana na mikopo ambayo serikali zilizopita ziliichukua kwa ajili ya maendeleo. Lakini sasa mikopo inatakiwa kulipwa na ile miradi ya maendeleo aidha haijaanza kutoa faida au fedha zilizokopwa zilitumika vibaya.
Na hii ndiyo hofu ya ukurasa huu kwa klabu ya Yanga na kinachoendelea chini ya utawala wa mhandisi Hersi Said.
Msimu wa 2022/23 klabu ya Yanga kupitia mkutano wake mkuu wa mwaka ilitangaza kwamba kulikuwa na MKOPO wa Sh4 bilioni uliorodheshwa kama sehemu ya mapato ya klabu.
Japo haikusemwa kwamba mkopeshaji ni nani, lakini ndiyo hivyo tena…mkopo ulishachukuliwa na kutumiwa.
Kwenye mkutano wa aina ileile wa mwaka huu haikusemwa kwamba deni lile limeshalipwa au la…na hakuna mwanachama aliyehoji.
Badala yake, mkurugenzi wa fedha wa klabu, Sabri Sadick, alipokuwa akisoma taarifa ya mapato na matumizi alisema kuna kiasi cha Sh5.45 bilioni kwenye bajeti mpya kinachotokana na MAPATO MENGINEYO.
Pesa hizo hazikufafanuliwa zilitokana na vyanzo gani, lakini hakukuwa na tatizo kwa sababu kwenye mambo ya bajeti kifungu hiki cha maneno MAPATO MENGINEYO ni cha kawaida.
Haya huwa mapato madogo madogo ambayo si rahisi kuorodhesha kila kimoja, hivyo hukaa kwenye lugha hiyo MAPATO MENGINEYO. Lakini hata hivyo, kwenye bajeti yoyote MAPATO MENGINEYO hayawezi kufika robo ya bajeti nzima.
Lakini kimsigi hiki cha Yanga kinafika robo ya bajeti yao…kwanini kiwekwe mwenye lugha hiyo ya kihasibu wakati wahasibu wote wa Yanga wanajua hilo?
Hapa panaibua maswali ya kidadisi kwamba yawezekana huu pia ukawa mkopo ambao Yanga waliuchukua kama ule wa msimu wa nyuma yake.
Na kama hivyo ilivyo, basi Yanga watakuwa na deni la Sh9.45 bilioni ndani ya miaka hii miwili ya mafanikio.
Hili deni ni lazima litakuwa na riba na kwa kadri linavyocheleweshwa kulipwa ndivyo riba inaongezeka.
Baada ya miaka mitano hata kama hawajaongeza mkopo mwingine, deni hilo linaweza kuwa mara mbili yake kutokana na riba.
Na hapo ndipo ilipo Kenya kwa sasa. Yale madeni waliyokopa miaka ya nyuma na kushindwa kuyalipa yakazaa riba kubwa iliyofanya yakue maradufu…na bado waliendelea kukopa.
Wakakopa hadi kufika kiwango cha mwisho cha kukopa. Wakawa hawakopesheki. Wakarudi kuwakamua wananchi nao wakagoma. Mitaa ikachafuka. Vipi hali hiyo ikitokea kwa Yanga. Madeni yote haya yatalipwaje?
Kuelekea msimu wa 2024/25 Yanga imeanza kufanya matumizi ya kufuru kwenye usajili.
Tayari wamefanikiwa kumbakisha nyota wao Aziz Ki kwa Shilingi za Tanzania zaidi ya milioni 500 huku akilipwa mshahara unaokaribia milioni 50 kwa mwezi.
Kwa mshahara huu, Aziz Ki ataikamua Yanga Sh600 milioni kwa mwaka mmoja kupitia mshahara.
Kwa ujumla msimu wa 2024/25 Aziz Ki ataigharimu Yanga Sh1.1 bilioni kwa kusaini mkataba na mshahara…hapo bado marupurupu mengine kama bonasi na kadhalika.
Yanga wamefanikiwa kumpata Prince Dube kwa kuwalipa Azam FC Sh540 milioni na yeye mwenyewe kupewa Sh300 milioni jumla ni Sh840 milioni.
Mshahara wa Dube ni Sh30 milioni kwa mwezi. Kwa mshahara huu, Dube ataikamua Yanga Sh360 milioni kwa mwaka.
Kwa ujumla msimu wa 2024/25 Prince Dube ataigharimu Yanga Sh1.2 bilioni kupitia fedha za kusaini mkataba na kumnunua na mshahara…hapo bado marupurupu mengine kama bonasi na kadhalika.
Na hawa ni wachezaji wawili pekee, bado Chama kama inavyotajwa, na wengine wengi. Huu ni mzigo mzito ambao Yanga inaubeba kama serikali ya Kenya ilivyobeba ujenzi wa SGR ya Nairobi – Mombasa.
Mzigo ukamuelemea punda…akautua kwa wananchi nao hawakukubali…wakaandamana.
Yanga inapaswa kuwa makini na matumizi yake japo wanapata mafanikio uwanjani. Kama kujifunza kutoka Kenya ni vigumu basi wajifunze kutoka kwa FC Barcelona.
Walihangaika kukopa mabilioni ili kumbakisha Lionel Messi na wakapata mafanikio uwanjani, lakini baada ya hapo mambo yamewageukia.
Mwaka 1997 Borussia Dortmund ya Ujerumani ilishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya. Nyota wao wakapanda thamani na klabu kubwa za Ulaya zikaanza kuwanyatia.
Ili kuwalinda, ikawapa mikataba minono wasiondoke na kweli hawakuondoka, lakini kimsingi klabu hiyo haikuwa na uwezo wa kuhimili gharama za mikataba ile. Ikafilisika hadi kushuka daraja. Yanga ijifunze kutoka huko, kama Kenya ni mbali.