Zigo la fedha lamng’oa Inonga Simba

BEKI wa Simba, Henock Inonga amebakiza hatua chache kujiunga na FAR Rabat ya Morocco baada ya timu hiyo kufuata saini yake.

FAR Rabat imezungumza na Simba ikitaka huduma ya beki huyo Mkongomani ambapo zimejadilianakufanya biashara na dau la zaidi ya Sh500 milioni linatajwa kufikiwa.

Inonga ambaye ana mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia Simba uamuzi wa kumuuza umekuja baada ya mabosi kuona dau walilowekewa linawashawishi huku kiwango cha chini uwanjani alichoonyesha msimu uliopita na majeraha yaliyomkabili ni sababu zingine zinazotajwa kuuzwa kwake.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kwamba, bodi ya klabu hiyo imeridhia kumuuza Inonga kwenda FAR Rabat kwa dau hilo.

“Simba tunachosubiri ni kuingizwa tu kwa fedha hizo kwani tayari tumeshakubaliana kila kitu. Bora aende huko tuwe na timu mpya kwa msimu ujao,” amesema bosi mmoja kutoka  ndani ya bodi ya klabu hiyo.

“Inonga ni beki mzuri kama ambavyo nilikwambia huko nyuma kwamba huu msimu uliopita umetuchafua sana, tukakosa raha. Ndio maana tulimtaka kama ana ofa ailete tumpe nafasi ya kuondoka kwa amani.”

Wakati Inonga akitajwa kuondoka Msimbazi tayari Simba imeshaanza msako wa haraka wa kutafuta beki mpya wa kati atakayechukua nafasi yake ikiendelea na mazungumzo na mabeki wa maana ikianza na Lameck Lawi wa Coastal Union.

Hata hivyo Simba imemsajili Lawi ikilipa sehemu kubwa ya gharama, lakini hivi karibuni Coastal Union imeibuka na kudai kuzuia dili hilo kwa madai kwamba vigogo wa Msimbazi walikiuka makubaliano ya awali.

Lawi ambaye ni beki mzawa, Simba pia inaangalia uwezekano wa kuwa na beki kutoka nje ya Tanzania ambpao miongoni mwa wanaotajwa ni Anthony Tra Bi Tra anayecheza ASEC Mimosas.

Ikumbukwe kuwa Inonga ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri katika michuano ya Afcon iliyopita akiwa na kikosi cha DR Congo, jambo lililosababisha timu mbalimbali kutamani huduma yake msimu ujao.

Akiwa Simba, Inonga ambaye alijiunga na timu hiyo Agosti 2021 amekuwa mchezaji muhimu katika eneo la beki wa kati akiingia kikosi cha kwanza moja kwa moja huku akifanikiwa kufunga mabao matano ndani ya Ligi Kuu.

Beki huyo anakumbukwa na wana Simba alipofunga bao kwa kichwa dakika ya pili dhidi ya Yanga pale Wekundu hao waliposhinda kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Aprili 16, 2023.

Mbali na kufanya mazuri ndani ya Simba ikiwemo kuisaidia kushinda Ngao ya Jamii msimu uliopita (2023-2024), lakini dakika za mwisho mwisho mwa msimu uliopita Inonga hakuwa na maelewano mazuri na uongozi wa klabu hiyo baada ya kuingia kwenye mgogoro wa kimkataba ambapo mwenyewe alidai unamalizika Juni 30, 2023 ilhali Simba wakisema utamalizika Juni 30, 2025.

Related Posts