Katika taarifa yake iliyotolewa kufuatia kauli ya waziri mkuu Netanyahu kuhusu makubaliano ya kumaliza vita hivyo, Jukwaa la familia za mateka na wasiojulikana walipo, limesema kukomesha mapigano Gaza bila kuwaachiwa mateka kutakuwa kushindwa kwa kihistoria kwa kitaifa na kuondoka kwenye malengo ya vita hivyo.
Wamesema wajibu na jukumu la kuwarejesha mateka viko mikononi mwa waziri mkuu, na kuongeza kuwa hakuna mtihani mkubwa kuliko huo.
Wakati wa shambulio la Hamas la Oktoba 7 kusini mwa Israel, wanamgambo waliwachukuwa mateka 251, ambapo 116 kati yao wanasalia Gaza, wakiwemo 41 ambao jeshi la Israel linasema wamekufa. Katika mahojiano yake ya kwanza na kituo cha televisheni cha nchini Israel, waziri mkuu Netanyahu alisema lengo kuu la vita linasalia kuwa kuwarejesha mateka na kuing’oa Hamas kutoka Gaza.
Soma pia: Msemaji wa jeshi la Israel asema Hamas haiwezi kusambaratishwa
Pia alisema yuko tayari kwa makubaliano ya usitishaji vita wa muda ili kufanikisha azma ya kuwarejesha mateka hao na kisha kuendeleza vita ili kufikia lengo la kuisambaratisha Hamas.
Pendekezo la kusitisha mapigano lililowasilishwa na Rais wa Marekani Joe Biden mwishoni mwa mwezi uliopita lilihimiza kuachiliwa kwa mateka na kufikiwa makubaliano ya usitishaji kamili wa vita.
Huku hofu ya kutokea kwa vita kamili nchini Lebanon ikiongezeka katika wiki za hivi karibuni, Netanyahu alisema Israel itawarejesha raia wake waliohamishwa kutoka jumuiya zao za kaskazini kwenye mpaka na Lebanon, kupitia diplomasia au kwa “njia nyingine”.
Alipoulizwa kuhusu mipango ya baada ya vita vya Gaza, alisema Israel itadumisha “udhibiti wa kijeshi katika siku zijazo” lakini kwamba “tunataka pia kuunda utawala wa kiraia, ikiwezekana wa Wapalestina wa ndani” na kuungwa mkono na mataifa ya kikanda.
Hamas ilikosoa vikali matamshi ya Netanyahu na kuyataja kama “uthibitisho wa wazi wa kukataa kwake azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pendekezo la Rais wa Marekani Joe Biden,” ambaye amehimiza kuachiliwa kwa mateka na kufikiwa kwa mapatano ya kusitisha vita.
Soma pia:UN yaishtumu Israel kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, Hamas kwa uhalifu wa kivitaHamas ilisisitiza kuwa makubaliano yoyote laazima yajumuishe usitishaji vita wa kudumu na uondoaji kamili wa wanajeshi wa Israel ili kukomesha kile ilichokiita “majaribio ya Netanyahu ya kukwepa, kuhadaa na kuendeleza uchokozi na vita vya maangamizi dhidi ya watu wetu”.
Annalena Baerbock kurudi Mashariki kwa mara ya nane
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock anasafiri kuelekea Tel Aviv siku ya Jumatatu kutokana na wasiwasi unaoongezeka kuhusu kuongezeka kwa mzozo kati ya Israel na kundi la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran la Hezbollah.
Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nje mjini Berlin, mazungumzo ya Baerbock nchini Israel na maeneo ya Wapalestina siku ya Jumanne yataangazia zaidi vita Gaza na janga la kibinadamu linaloendelea huko.
Soma pia: Hofu ya vita kamili kati ya Israel na Hezbollah yaongezeka
Kama ilivyokuwa kwenye ziara zake za huko nyuma, Baerbock amesema suluhisho la mataifa mawili litakuwa ajenda ya mazungumzo. Mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Israel Israel Katz umepangwa kufanyika Jerusalem.
Siku ya Jumanne, mazungumzo yamepangwa mjini Ramallah na waziri mkuu wa Mamlaka ya Palestina (PA), Mohammed Mustafa, kuhusu hali ya Ukingo wa Magharibi na juhudi za mageuzi za PA.
Jumanne jioni, Baerbock anapanga kuzungumza na Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut.
Akizungumza mjini Luxembourg alikohudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, waziri Baerbock alisisitiza haja ya kusitisha mapigano Gaza.
Soma pia:Israel, Hizbullah washambuliana tena
”Usitishaji huu wa mapigano ni suala la dharura zaidi kuliko hapo awali na katika muktadha huu, ninasafiri huko na pia Lebanon kwa sababu hali huko ni ya wasiwasi mkubwa. Kuongezeka zaidi kunaweza kuwa janga kwa kila mtu katika eneo hilo, ndiyo maana ni muhimu sana hatimaye tupate muafaka wa kusitisha vita Gaza.”
UNRWA yapambaniwa uwepo wake
Wakati huo mapambano makali yanaendelea Gaza ambapo wizara ya afya ya ukanda huo imeripoti kuwa Wapalestina wapatao 37,626 wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu Oktoba 7.
Idadi hiyo inajumuisha takriban vifo 28 katika muda wa saa 24 zilizopita, taarifa ya wizara hiyo ilisema, ikiongeza kuwa watu 86,098 wamejeruhiwa.
Hayo yakijiri, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, Philippe Lazzarini, ameyatolewa wito mataifa wanachama kusimama na shirika hilo kukabiliana na juhudi za Israel kutaka kulivunja, na kuonya kuwa ikiwa UNRWA itavunjwa, mashirika mengine yatafuta na hivyo kudhoofisha mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa.
Soma pia: Ujerumani kuanza tena ushirikiano na shirika la Palestina UNRWA
“Israel kwa muda mrefu imekuwa ikikosoa mamlaka ya shirika hilo. Lakini sasa inalenga kusitisha oparesheni za UNRWA, ikitupilia mbali hadhi ya shirika hilo kama shirika la Umoja wa Mataifa linaloungwa mkono na mataifa mengi wanachama,” alisema Lazzarini katika mkutano wa tume ya ushauri ya shirika hilo mjini Geneva.
“Ikiwa hatutapambana, mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa yatafuata, na kudhoofisha mfumo wetu wa kimataifa.”
Lazzarini alisema shirika hilo, ambalo limetoa msaada muhimu kwa wakaazi wa Gaza katika kipindi chote cha mashambulizi ya Israel, lilikuwa “linayumba kutokana na uzito wa mashambulizi yasiyokoma”.
Katika Ukanda wa Gaza, shirika hilo limelipa gharama kubwa ambapo kulingana na Lazzatini, watumishi wake 193 wameuawa, huku vituo vyake 180 vikiharibiwa au kuvunja kabisaa, na watu wasiopungua 500 waliokwenda kutafuta ulinzi wa Umoja wa Mataifa wakiuawa.