Mnigeria afunguka dili la Simba

KIUNGO mkabaji wa Rivers United, Mnigeria Augustine Okejepha ameeleza dili lake la kujiunga na Simba, huku akisisitiza shauku yake kubwa ni kucheza soka la Tanzania licha ya kuwa na ofa kutoka klabu zingine nje ya nchi hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Nigeria, Okejepha amesema ni kweli wako katika mazungumzo na viongozi wa Simba, lakini bado hajasaini mkataba wa kuichezea msimu ujao.

“Ni kweli tuko katika mazungumzo, ila siwezi kusema moja kwa moja kwa sasa kwa sababu bado hatujafikia uamuzi wa mwisho. Napenda sana kucheza Tanzania kwani ni ligi yenye ushindani ambayo imekuwa ikivutia nyota wengi kujiunga nayo,” amesema.

Mnigeria huyo mwenye umri wa miaka 20, amesema mbali na Simba inayomtaka, lakini kuna ofa zilizo mezani kwa uongozi wa timu anayoichezea ikiwemo ya FC Ural Yekaterinburg kutoka Urusi inayoshiki Ligi Daraja la Kwanza. “Wapo wachezaji wengi kutoka Nigeria ambao walipita au wapo hadi sasa hivi katika soka la Tanzania kama Nelson Okwa (aliwahi kucheza Simba sasa Plateu United ya Nigeria), Victor Akpan (kakipiga Coastal Union na Simba sasa ni mchezaji huru), Benjamin Tanimu na Morice Chukwu (Singida Black Stars), hivyo nami napenda kuona nikiwa sehemu kama hiyo,” amesema.

Okejepha aliyewahi kuchezea Kano Pillars aliyojiunga nayo akitokea Warri Wolves FC zote za Nigeria, ameongeza kuwa baada ya Ligi Kuu nchini kwao kumalizika juzi, atakutana na wawakilishi wake kabla ya kufanya uamuzi atakapokwenda.

Mwanaspoti iliripoti hivi karibuni juu ya dili hilo la Simba na Mnigeria huyo anayetajwa kuchukua nafasi ya Msenegali Babacar Sarr anayetarajiwa kuachwa muda wowote ili kupisha majembe mengine mapya kuanza kuingia Msimbazi.

Tayari Simba imeshatangaza kuachana na wachezaji na nahodha wa timu hiyo, John Bocco, Shaaban Idd Chilunda, Saido Ntibazonkiza ‘Saido’ na Kennedy Juma huku ikimtambulisha beki wa kati, Lameck Lawi kutoka Coastal Union.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia juu ya usajili huo alikaririwa akisema wakati huu ni wa usajili na kila mchezaji anatajwa kujiunga na timu hiyo na kwamba hawawezi kujibu kila kitu  kinachoendelea.

“Hili ni dirisha la usajili na mengi yanazungumzwa.  Nikisema nizungumzie kila mchezaji anayetajwa kutua Simba nitachoka. Naomba hili tuliache kwanza kwani muda wa kutambulisha wachezaji tuliowasajili ukifika tutafanya hivyo,” alisema Ahmed.

Okejepha ameonyesha kiwango bora akiwa na Rivers United ambapo ameiwezesha kumaliza msimu ikiwa katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Nigeria (NPFL) na pointi 53, baada ya kushinda michezo 15, sare nane na kupoteza 15.

Katika ligi hiyo, Enugu Rangers imetwaa ubingwa baada ya kushinda michezo 21, sare saba na kupoteza 10 ikikusanya pointi 70 nyuma ya Remo Stars iliyoshika nafasi ya pili na pointi 65, huku Enyimba ikimaliza ya tatu na pointi 63.

Related Posts