TAARIFA zinabainisha kwamba, ile filamu ya Clatous Chama na Simba imefikia mwisho baada ya mchezaji huyo mkataba wake kumalizika na ishu ya kuongezewa muda wa kusalia Msimbazi ikishindikana, huku ishu mpya ikiwa namna pande hizo zilivyomalizana.
Kiungo huyo raia wa Zambia, alikuwa kwenye majadiliano marefu na viongozi wa Simba akiwemo Mwenyekiti wa Bodi na rais wa heshima wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’.
Katika majadiliano hayo ndiko yameibuka majibu ya kiungo huyo kutoendelea kuitumikia Simba msimu ujao huku ikielezwa tayari amepewa mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Yanga.
Chama ambaye Januari 14, 2022 alirejea Simba akitokea RS Berkane, inaelezwa sababu kubwa ya kutoongezewa mkataba klabu hapo ni ishu ya maslahi.
Chanzo kutoka ndani ya Simba kimebainisha kwamba katika majadiliano baina ya Chama na uongozi wa klabu hiyo, kila upande ulikuwa ukivutia upande wake na mwisho wa siku hawakufikia muafaka mzuri.
“Simba walitaka kubaki na Chama na mchezaji mwenyewe alionyesha nia ya kubaki, tatizo lilikuja katika ishu ya maslahi ambapo kila upande uliweka mapendekezo yake,” kimeeleza chanzo hicho.
“Chama alitaka kupewa dola laki mbili ili asaini mkataba mpya wa mwaka mmoja, jambo ambalo viongozi wa Simba hawakukubaliana nalo.
“Viongozi wa Simba wao walitaka kumpa Chama kiasi hicho cha fedha ambacho ni dola laki mbili lakini asaini mkataba wa miaka mitatu, mchezaji akakataa. Ishu ikaishia hapo.”
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amezungumzia ishu ya Chama akisema: “Mpaka sasa mimi kama msemaji bado sijapata uhalisia wa kipi kinaendelea endapo ameongezewa mkataba au viongozi wameamua aondoke ama mazungumzo bado yanaendelea. “Likishamalizika kwa ngazi ya juu uongozi unanipa taarifa au watatoa taarifa na Wanasimba wapate kufahamu kipi kinaendelea juu ya Mwamba wa Lusaka.”
Mara ya kwanza alipotua nchini Chama alitambulishwa kuwa mchezaji wa Simba, Julai 2018 akitokea Lusaka Dynamos FC ya kwao Zambia kabla ya kurejea tena Januari 2022.
Ndani ya Simba, Chama amecheza kwa misimu minne na nusu akishinda mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara, huku akiwa katika mafanikio ya timu hiyo ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne (2018–19, 2020–21, 2022–23 na 2023-2024).