Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema anawaunga mkono wafanyabiashara wa Kariakoo walioanza mgomo jana Jumatatu kuishinikiza serikali kutatua changamoto zao na kuwaomba wafanyabiashara wengine Tanzania nzima waungane na wenzao. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akihutubia wananchi na wafuasi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Monduli jana, Mbowe amesema inabidi wafanyabiashara hao waungwe mkono ili serikali ijue namna wananchi walivyo na hasira kutokana na ugumu wa maisha.
“Wafanyabiashara wa Kariakoo wanasema kodi zimekuwa kubwa, wananchi wanashindwa kununua bidhaa, Serikali ipunguze kodi tunaua mitaji yetu. Tunawaunga mkono wafanyabiashara wa Kariakoo, tunawaomba wafanyabiashara wengine Tanzania nzima tufike mahali tuikatae hii Serikali ya wahuni,” amesema Mbowe na kuongeza;
“Hasira za namna hii ndio hicho watoto wa Kenya wanachofanya. Wakati tozo ya simu na miamala inaanzishwa, Watanzania tuliangalia lakini Wakenya wanajitambua wameandamana mpaka serikali imekubali kuondoa.
“Hii mijamaa inakopa sana kwa sababu zaidi ya asilimia 51 ya bajeti ya serikali ni kulipa madeni. Hawana namna ya kuendesha serikali ndio maana lazima walete mzigo kwenu na hatujui fedha waliyokopa wamefanyia nini kwa sababu mikataba yote ya serikali ni siri… tumebaki kukopa Jumatatu mpaka Alhamisi,” amesema.
Amesema mifumo ya kodi inaua mitaji ya wafanyabiashara wengi na kusababisha ugumu wa maisha kwa watanzania.