Wafanyabiashara Mwanza waanika sababu za kufunga maduka yao

Mwanza. Wakati wafanyabiashara jijini Mwanza wakitangaza mgomo na kufunga maduka yao, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati ametaja sababu za mgomo huo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Juni 25, 2024, Masagati ametaja sababu hizo kuwa ni kupinga sheria za kodi (bila kuzitaja) zinazochangia unyonyaji na kuwarudisha nyuma wafanyabiashara.

“Kitu ambacho kimewasukuma wafanyabiashara kusitisha biashara zao ni yale yanayoendelea kuhusiana na sheria za kodi. Sheria za kodi zimekuwa tatizo,” amesema Masagati.

Alipoulizwa ukomo wa mgomo huo, Masagati amesema hawezi kuweka wazi lini utakoma kwa kile alichodai jukumu la kusitisha mgomo huo limekabidhiwa mikononi mwa wafanyabiashara wenyewe.

“Baada ya kuwasilisha kero na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara kwenye mamlaka za Serikali na kurejesha tuliyoyapata serikalini, kwa hiyo wameona hatua zaidi ya kuchukua ni kusitisha biashara zao,” amesema Masagati.

Baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira

 “Malalamiko na matamanio ya wafanyabishara ni kuona sheria zinazosimamia wafanyabiashara zinarekebishwa. Na kwa sababu leo Waziri wa Fedha anawasilisha bajeti ya Taifa, tunaamini kwamba yale ambayo wafanyabiashara wanayalalamikia yatarekebishwa,” amesema Masagati.

Uamuzi wa wafanyabiashara kufunga maduka yao umeacha maumivu kwa wafanyabishara wadogo ‘Machinga’ na wachuuzi wa bidhaa kutoka mikoa ya jirani na Mwanza ambao wamesafiri umbali mrefu kununua bidhaa jijini humo na kukutana na ‘makufuli’ katika milango ya maduka.

Machinga kutoka wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, Enock Timba amesema mgomo huo umemsababishia athari kwa kile alichodai pamoja na kufika katikati ya jiji saa 12:30 asubuhi kwa lengo la kununua bidhaa, ameishia kuzunguka tu bila kuona duka lililofunguliwa.

“Sikutegemea kama nitakutana na mgomo nimeathirika sana, inabidi nizunguke sijui maduka yamefunguliwa wapi hata hivyo ninakoelekea sasa ni kurudi nyumbani sioni dalili za maduka kufunguliwa,” amesema Timba.

Mkazi wa Nyasaka jijini humo, Maria Nzemba amesema hofu yake ni namna gani atarejesha mkopo aliochukua kwa ajili ya kuanzisha biashara yake kwa kile alichodai amekosa bidhaa za kuzungusha katika eneo lake.

“Kwa kweli siku ya leo imetuathiri sana wafanyabishara wadogo, tuna mikopo, tuna watoto wanasoma na shule zinaenda kufunguliwa, maduka makubwa ambayo tunayategemea kununua bidhaa ili tuanze kuzungusha mitaani yamefugwwa tunaomba Serikali ifuatilie suala hili,” amesema Maria.

Mussa Fundikila kutoka Wilaya ya Chato mkoani Geita ameeleza kushangazwa na uamuzi huo wa wafanyabiashara huku akiumizwa kusafiri umbali mrefu hadi Mwanza na kukutana na mgomo huo.

Hadi kufikia saa 5:50 asubuhi, Mwananchi imeshuhudia hakuna dalili za wafanyabiashara kufungua maduka huku jitihada za kutafuta kauli ya Serikali kuhusiana na mgomo huo zikiendelea.

Endelea kufuatilia Mwananchi Digital.

Related Posts