Mastaa kibao Tabora United kuchapa lapa

LICHA ya Tabora United kubaki Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao, lakini inaelezwa mastaa wengi wa kikosi hicho huenda wakaondoka na kutafuta changamoto sehemu nyingine, huku sababu kubwa ikielezwa kuwa ni ukata unaoikumba timu hiyo.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo zimeiambia Mwanaspoti kwamba baadhi ya nyota ambao wataondoka ni kipa raia wa Nigeria, John Noble aliyetokea Enyimba na mshambuliaji Mghana Eric Okutu aliyejiunga akitokea Hearts of Lions.

Okutu aliyefunga mabao saba katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita huku akiwa ndiye kinara katika timu hiyo, inaelezwa ameanza mazungumzo na klabu mbalimbali na licha tu ya kubakisha mkataba wa mwaka mmoja, lakini inaelezwa kwamba yupo tayari kuuvunja.

“Ni kweli baadhi ya wachezaji wetu wameonyesha kuondoka na hawatokuwa sehemu ya kikosi, nyota kama John (Noble), Eric Okutu na Ben Nakibinge ni miongoni mwao wanaotaka kuondoka ingawa bado tunapambana kuwabakisha,” kimesema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Tabora United, Christina Mwagala amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote na viongozi wanachofanya kwa sasa ni kulipa fedha wanazodaiwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) ili wafunguliwe kusajili.

“Tumetoa mapumziko kwa wachezaji baada ya kujihakikishia kubaki Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao. Mchezaji anapodai haina maana kwamba anavunja mkataba wake, hivyo tunapambana kulipa fedha tunazodaiwa na Fifa kisha tutaongea mengine,” amesema.

Timu hiyo yenye maskani yake mjini Tabora ilijihakikishia kubaki Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Biashara United ya Musoma mkoani Mara kufuatia kumaliza msimu ikiwa katika nafasi ya 14 na pointi 27.

Related Posts