Arusha. Mahakama ya Rufani, imebatilisha mwenendo wa kesi kufuta hukumu ya kifungo cha miaka 15 jela aliyohukumiwa Lufino Gabriel kwa kukutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola 1,500 za Marekani baada ya kubaini dosari za kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo.
Imeamuru kesi hiyo kusikilizwa upya kwenye Mahakama yenye uwezo baada ya kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na wakati huohuo mrufani atasalia kizuizini akisubiri kusikilizwa tena.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja ya Wakili wa Jamhuri aliyeomba Mahakama hiyo kutumia mamlaka yake kubatilisha mwenendo wa Mahakama ya awali,kufuta hukumu iliyotolewa kwa mrufani pamoja na kuamuru shauri kuanza upya.
Rufaa hiyo ya jinai namba 652/2022 ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Rehema Mkuye, Lucia Kairo na Lameck Mlacha, waliotoa uamuzi huo Juni 21, 2024.
Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro Machi 17, 2023 katika kesi ya jinai namba 108/2022.
Hii ni rufaa ya pili, mrufani na mtu mwingine ambaye si mhusika katika rufaa hiyo walishtakiwa kwa kumiliki nyara za Serikali kinyume cha kifungu cha 86 (1), (2) (b) na (3) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.
Kifungu hicho kilisomwa kwa pamoja na ibara ya 14 ya jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Kuratibu, Sura ya 200 (EOCCA).
Shtaka la pili lilikuwa ni umiliki wa silaha ya moto kinyume na Sheria, lililomhusu Germanus Iddi aliyekuwa mshitakiwa wa pili ambaye baadaye aliachiwa huru na Mahakama ya Awali baada ya kubaini upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi yake.
Walidaiwa Julai 19, 2017, eneo la Live Green Lodge, Kijiji cha Mlimba wilayani Kilombero mkoani Morogoro, walikutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za 1,500 Marekani bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.
Ili kuthibitisha mashitaka hayo jamhuri ilikuwa na mashahidi 11,vielelezo vitano huku mrufani na mwenzake wakijitetea chini ya hati ya kiapo,
Mwenzake aliachiwa huru na Mahakama na mrufani kukutwa na hatia na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 15 jela.
Baada ya hukumu hiyo, mrufani huyo alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, jaji aliyesikiliza alithibitisha kukutwa na hatia hiyo lakini alibaini kuwa, kifungo cha miaka 15 jela kilikuwa na makosa.
Kwa hiyo, aliiongeza hadi kifungo cha miaka 20 kwa mujibu wa kifungu cha 60 (2) (a) cha EOCCA.
Karika rufaa hiyo mrufani aliwakilishwa na Wakili Daudi Mkilya huku akiwa na sababu 12 za rufaa, na mjibu rufaa (jamhuri), akiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Upendo Shemkole.
Kabla ya kuanza kusikiliza kesi hiyo, Mahakama ilitaka kuthibitisha uhalali wa ridhaa ya DPP na cheti chake kinachoonekana katika ukurasa wa saba na nane wa rekodi ya rufaa na kuwaalika mawakili wa pande zote kushughulikia suala hilo.
Wakili Mkilya alieleza kuwa Mahakama iliyosikiliza na kuamua shauri hilo haina mamlaka ya kufanya hivyo, kwa kuwa hapakuwa na ridhaa wala cheti sahihi kinachotoa mamlaka kwa Mahakama ya awali iliyotoa hukumu ya miaka 15 kwa mrufani.
Alidai kuwa hati hiyo haikutaja masharti mahsusi ambayo mrufani alipaswa kushtakiwa, kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mrufani anadaiwa kukiuka kifungu cha 86 1(1), (2) (b) na (3) cha Sheria ya Wanyamapori.
Alidai kwa kushindwa kutaja kifungu ambacho mrufani alipaswa kushtakiwa, kiliathiri mamlaka ya Mahakama iliyokusudiwa kusikiliza na kuamua shauri hilo, hivyo mwenendo mzima na uamuzi uliotokana na hilo ulikuwa batili.
Alieleza katika mazingira hayo Mahakama hiyo ya rufani inaweza kubatilisha shauri,kufuta mwenendo na hukumu.
Naye Wakili Shemkole alikiri ridhaa hiyo ya DPP haikutoa mamlaka kwa Mahakama inayosikiliza na kuamua shauri hilo kutokana na kutonukuu kifungu maalumu cha sheria chini ya ambayo mrufani alishtakiwa.
Wakili huyo aliiomba Mahakama kutumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 4 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufani kubatilisha mwenendo mzima wa shauri katika Mahakama ya awali, kufuta hukumu iliyotolewa kwa mrufani.
Baada ya mawasilisho ya pande zote, majaji walianza kwa kuangalia iwapo Mahakama ilitekeleza wajibu wake bila kuwa na mamlaka na kama ilivyowasilishwa na pande zote,ridhaa ya DPP haikueleza kifungu cha sheria ya makosa inayomkabili mrufani.
Wameeleza kuwa ni msimamo wa kisheria kuwa ridhaa ya DPP na cheti kinachoruhusu mamlaka ya Mahakama ya chini kusikiliza kesi iliyopaswa kusikilizwa na Mahakama ya juu lazima kitolewe kwa kuzingatia masharti ya shtaka hilo.
Huku wakinukuu shauri lililotolewa uamuzi na Mahakama ya rufani, majaji walieleza katika kesi ya DPP hakutaja vifungu vya sheria vinavyounda makosa ya kiuchumi.
Wameeleza kuwa kutonukuu kifungu mahsusi kunamaanisha kuwa mrufani na mshtakiwa aliyeachiwa huru, walishtakiwa, kuhukumiwa na kutiwa hatiani na Mahakama ya chini bila kibali cha DPP na zaidi bila mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Majaji hao wamefafanua ni msimamo wa kisheria kuwa ridhaa ya DPP na cheti kinachotoa mamlaka kwa Mahakama ya chini kuhukumu kesi ya uhalifu wa kiuchumi lazima itolewe kwa kuzingatia masharti hayo, vinginevyo inakuwa batili.
Wameeleza kuwa kutokana na dosari hizo sisizoweza kutibika kama ilivyoainishwa na mawakili wa pande zote mbili, kwa sababu hiyo, wamebaini kuwa mashauri yote ya Mahakama za chini yalikuwa batili.
“Tunaomba mamlaka yetu ya marekebisho chini ya kifungu cha 4 (2) cha AJA kubatilisha kesi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro,” amesema.
“Hatia ya matokeo na hukumu pamoja na mwenendo wa Mahakama Kuu, Masijala ndogo ya Morogoro ambayo iliridhia mashitaka hayo kinyume cha sheria, tunatengua hukumu ya mrufani na kuweka kando hukumu aliyopewa,” wameeleza majaji hao.
Kuhusu hoja ya kuamuru kusikilizwa upya kwa kesi hiyo, walieleza kutokana na ukiukwaji huo uliotajwa kufanya mwenendo mzima wa Mahakama ya awali kuwa haramu,kesi hiyo inatakiwa kusikilizwa upya kwa mrufani na mwenzake aliyeachiwa huru, Germanus Idd.
“Amri ya kusikilizwa upya itahusisha kusikilizwa upya kwa watuhumiwa wote wawili, hakuna mtuhumiwa hata mmoja atakayenyimwa haki ya kusikilizwa, hivyo tunaamuru kesi hiyo isikilizwe upya, kwa cheti sahihi kinachotoa mamlaka ya kibali kutoka kwa DPP,” wameeleza.
Aidha, wamesema wakati huo mrufani atasalia kizuizini akisubiri kusikilizwa tena na kuamuru ikiwa mrufani atapatikana na hatia na kuhukumiwa, muda aliotumikia kifungo ujumuishwe kwenye kifungo atakachoadhibiwa nacho.