Na Mwandishi Wetu, Ifakara
MKUU wa mkoa wa Morogoro ,Adam Malima amekemea vikali kuwepo kwa migogoro na migongano isiyokwisha ya viongozi wa halmashauri ya mji wa Ifakara ambayo imekua ni chanzo cha kudhorotesha kwa kutokamilika miradi ya maendeleo ya huduma za kijamii na kiuchumi.
Malima amesema hayo wakati wa kikao cha Baraza maalum la Madiwani wa halmashauri ya mji huo la kupitia na kujadili hoja nane za ukaguzi zilizoibuliwa na Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikli (CAG).
Amesema kuna baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wanaendekeza majungu na migongano hata kwa kiongozi wao ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, kwa watu kushindwa kutekeleza vema majukumu yao na kusababisha halmashauri kuzidi kuzama.
” Wapo baadhi ya watendaji na wakuu wa idara mbalimbali hamtekelezi maagizo mnayopewa mkurugenzi wenu mnataka kumwamisha na tumewabaini na tutachukua hatua , mkurugenzi na wewe simamia halmashauri , kaa vyema na madiwani uwasikilize ushauri wanakupatia na mshirikiane kuketa mandeleo ya wananchi” alisisitiza Malima.
Malima amesema kuwa mivutano na migogoro hiyo imechangia zaidi ya miradi saba ya maendeleo ambayo Serikali kuu imetoa fedha nyingi kushindwa kukamilishwa kwa wakati na kuwanyima haki wananchi kunufaika na huduma za kijamii kama maji, elimu na afya kwa wakazi wa mji huo .
” .. Mimi nikiwa mkuu wa mkoa siwezi tukakaa kimya huku Ifakara inazama , watumishi na madiwani wanamagomvi …. madiwani mnamagomvi hamsimamii miradi haiwezekani..” amesema Malima .
Mkuu wa mkoa amewataja watumishi wa halmashauri hiyo pamoja na madiwani kujitathimini wao kama wapo kwa maslahi yao binafsi na kama hivyo waache mara moja bali wafanye kazi kwa maslahi ya umma na kuwaletea wananchi maendeleo wanayohitaji.
” Kama wewe ni diwani nenda kajitathimini uko upande wa Diwani maendeleo au uko upande wa Diwani maslahi binafsi, kama wewe ni mtendaji kajitathimini, kama wewe ni mtendaji maendeleo au mtendaji maslahi binafsi” amesema Malima .
Mkuu wa mkoa pia aliwakata madiwani hao na watendaji wa halmashauri hiyo kuhakikishwa wanaongeza nguvu katika suala la ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumi yake .
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara ,Kassim Nakapala ameonesha masikitiko yake ya kutokamilika kwa wakati ujenzi wa jengo la Ofisi ya za utawala wa Halmashauri uliochukua zaidi ya miaka saba na linalogharimu zaidi ya sh bilioni 7.4 ambapo ujenzi unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Licha ya kuelezea jambo hilo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kwa kuiwezesha kifedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa maji utakaowezesha kuwaondolea changamto wananchi wa Mji wa Ifakara.
Kwa upande wake , Katibu Tawala wa Mkoa huo Dk Mussa Ali Musa ametumia fursa hiyo kuwataka wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kupeleka Benki fedha zote za makusanyo katika Halmashauri zao kabla au ifikapo Juni 30, 2024.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro ,Adam Malima akisisitiza
jambo kwenye kikao
cha kupitia na kujadili hoja nane za ukaguzi zilizoibuliwa na Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za
serikli (CAG) wakati wa Baraza maalum la Madiwani wa halmashauri ya mji Ifakara.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro ,Adam Malima ( kati
kati) akiendesha kikao cha kupitia na kujadili hoja
nane za ukaguzi zilizoibuliwa na Mdhibiti
na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikli (CAG) kwenye Baraza maalum la Madiwani wa halmashauri ya
mji Ifakara na (wapili kutoka kushoto)
ni Katibu Tawala wa mkoa huo, Dk Mussa Ali Mussa , wakati ( wakwanza kushoto)
ni Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Dustan Kyobya, wakati wapili ( kulia) ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Zahara Michuzi akifuatiwa na
Mwenyekiti wa halmashauri ,Kassim Nakapala.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Ifakara , Zahara Michuzi akiwa
pamoja na Mwenyekiti wake wa halmashauri ,Kassim Nakapala ( kushoto) pamoja
na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo aliyeketi kulia.( Picha na Mwandishi
Wetu).