RC Batilda aagiza Halmashauri Lushoto kulipa madeni

Lushoto. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kulipa deni la zaidi ya Sh700 milioni, linalodaiwa na wafanyakazi, makandarasi na watoa huduma wengine.

Amesema deni hilo linaonyeshwa kwenye vitabu vya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hayo amesema leo Jumanne Juni 25, 2024  wilayani Lushoto kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani lililokuwa linajadili hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Balozi Burian amesema watumishi na watoa huduma wengine wanatakiwa kulipwa fedha zao, haoni sababu ya wakurugenzi na wahasibu kuendelea kuzikalia.

“Tunayo tabia waliokuwepo kwenye kitengo cha malipo cha fedha kuona kwamba haya madeni ni kama vile unamfanyia mtu upendeleo, deni la mtu sio upendeleo. Ukitaka kujua uchungu vaa viatu vyake. Madeni ya watumishi yalipwe. Kuna deni la watumishi lenye thamani ya Sh763,182,290 ambalo halijalipwa mpaka sasa na hilo ndio imesababisha hoja namba 2.2.2 kwenye kitabu cha CAG, naomba lilipwe haraka,” amesema Burian.

Akitoa taarifa yake kwenye barazani hapo, Mkaguzi wa Nje wa Mkoa wa Tanga, Hamu Mwakasola amesema Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa mwaka wa fedha 2022/23, imepata hati inayoridhisha.

Amesema hiyo inatokana na utekelezaji wa mapendekezo 27 sawa na asilimia 47 waliyojiwekea.

Hata hivyo, amesema mapendekezo 30 sawa na asilimia 53 yameendelea kusalia bila kupata majibu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema amesema Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa miaka mitatu iliyopita, ilikuwa haifikishi hata asilimia 90 ya mapato yake.

Amesema mara nyingi walikuwa wakifikia ukomo wa ukusanyaki wa mapato kwa asilimia 85 lakini hivi sasa wamevuka na wanafikisha asilimia 90.

Amewataka viongozi kuongeza juhudi zaidi za kukusanya mapato, kwa sababu hakuna shughuli yoyote ya Serikali itaweza kufanyika bila ya kukusanya mapato.

Kwa mwaka wa fedha 2022/23, katika halmashauri 11 za Mkoa wa Tanga, kumi zimepata hati safi, huku Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ikiwa imepata hati yenye mashaka.

Related Posts