Benki ya NMB Yafanikisha Maonesho ya Pili ya Kimataifa – Sekta ya Mifugo – MWANAHARAKATI MZALENDO

Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameipongeza Benki ya NMB kwa kuanza kutoa bima ya mifugo inayolenga kupunguza hatari kwa wafugaji kote nchini.
Bidhaa hii ya bima ni sehemu ya dhamira ya benki hiyo ya kuwalinda wafugaji dhidi ya hasara za kifedha zinazoweza kutokea kwa wafugaji zikiwemo hatari za ghafla au zisizotarajiwa.
Akizungumza kwenye banda la benki hiyo wakati wa kufunga maonyesho ya siku tatu ya Mifugo yaliyoandaliwa na Chama cha Wafugaji Kibiashara (TCCS) na kufadhiliwa na Benki ya NMB na kukutanisha na wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo mwishoni mwa wiki, Biteko alisema kuwa bima ya mifugo ni dhana mpya katika soko la Tanzania na kuitaka benki hiyo kuongeza wigo wake ili kuwanufaisha wafugaji wengi nchini.
“Kwa kweli nimeifurahia hii dhana ya bima ya mifugo na nakiri kwamba ni dhana mpya katika soko la Tanzania,” alisema.
Biteko alisema ingawa idadi ya ng’ombe imeendela kukua siku hadi siku na kufikia milioni 37 katika miaka ya hivi karibuni, mchango wa sekta ya mifugo katika uchumi wa nchi bado ni mdogo sana.
“Hii ni kwa sababu ya kutegemea ufugaji wa ng’ombe wa kizamani. Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatakiwa kuja na mikakati mipya ya kuwawezesha wafugaji kubadili ufugaji na kuwawezesha kufuga kisasa,” alisema.
Biteko alisema tayari Serikali imekamilisha Mpango Kabambe wa Sekta ya Kilimo unaolenga kutatua changamoto kadhaa zinazoendelea kukwamisha maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo nchini.
“Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo,” aliongeza.
Awali, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Wateja Wakubwa ya Benki ya NMB, Christopher Mwalugenge alisema bima ya mifugo inayotolewa na benki yake inajumuisha aina kadhaa za hatari zinazohusiana na mifugo, zikiwemo vifo na wizi wa mifugo.
“Kama benki, tunaelewa kuwa mifugo ni vitega uchumi muhimu hivyo ilikulinda wafugaji dhidi ya upotevu wa ghafla, tumekuja na hii bima mifugo ambayo inaghariu kiasi cha shilingi elfu 20 tu kila mfugo kwa mwaka,”
Aliongeza kuwa benki yake imejikita katika kulinda vitega uchumi vya wafugaji kwa kutoa bima ya mifugo iliyoboreshwa ili kupata mustakabali wa mifugo yao pamoja na mustakabali wa biashara zao.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti wakati wa hafla hiyo aliwataka wafugaji kuachana na ufugaji wa asili na kuanza ufugaji wa kisasa ili kuleta tija katika biashara zao.
“Kama wizara, tumekuwa tukitoa elimu na kuhamasisha wafugaji kuachana na ufugaji wa kizamani na kuanza kufuga kisasa lakini mwitikio bado ni mdogo sana. Wafugaji wengi nchini Tanzania wanaendelea kutegemea ufugaji wa asili ambao unadhoofisha tija.  Siku zimepita ambapo mfugaji anasafiri umbali mrefu kutafuta malisho,” alisema.

MWISHO

 

 

Related Posts