SMZ kutobinafsisha sekta ya elimu, ZSTC

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema haina mpango wa kubinafsisha sekta ya elimu na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kutokana na umuhimu wake na unyeti kwa masilahi ya Taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma ametoa kauli hiyo Juni 25, 2024 akijibu swali la mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad katika baraza la wawakilishi Chukwani.

Profesa Hamad alitaka kujua mpango wa Serikali kubinafsisha taasisi hizo katika kuleta utendaji wenye ufanisi.

“Kwa sasa Serikali haina mpango wa kuibinafsisha sekta ya elimu hasa tukizingatia tupo katika utekelezaji wa mageuzi ya elimu ambayo yanalenga kuimairisha sekta hiyo. Katika mpango huu wa mageuzi Serikali imedhamiria kuimarisha ushirikishwaji wa sekta binafsi katika maendeleo ya aekta badala ya kubinafsisha moja kwa moja,” amesema.

Kuhusu ZSTC, Waziri Hamza amesema shirika hilo ndilo mkombozi wa pekee ambalo limeweza kulisimamia zao la karafuu na kuzinunua kutoka kwa wakulima kwa bei nzuri na hata pale ilipotokea bei ya karafuu kuporomoka katika soko la dunia.

“Mwaka 2019/2020 Serikali kupitia ZSTC haikushusha bei kwa wakulima, shirika lilifanya hivyo kwa lengo la kuwatia motisha wakulima wa zao hili ili waweze kuliimarisha zaidi na kunufaika nalo,” amesema.

Wakati huohuo, SMZ imepata Sh2 bilioni kutokana na usajili wa magari kisiwani humo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2020 hadi 2023.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Mohammed alipojibu swali la mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman wakati wa mkutano wa 15 wa baraza la wawakilishi Juni 25, 2024.

Katika swali la msingi la Dk Mohammed, alitaka kujua mapato Serikali inayoingiza kwa mwaka kutokana na usajili wa namba za vyombo vya moto Zanzibar. Pia, alitaka kujua mfumo na utaratibu wa utoaji wa namba za usajili katika vyombo vya moto unaotumika.

Waziri Khalid katika majibu amesema Serikali inatumia mfumo wa usajili wa vyombo vya moto unaojulikana “motor vehicles registration system’ unaotekelezwa kupitia Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).

Kuhusu utaratibu amesema muhusika anayeingiza chombo cha moto nchini hatakiwa kuwasilisha vielelezo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baadaye kupelekwa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) ambao humpatia taarifa za chombo hicho, ambazo hupelekwa ZRA kwa ajili ya kupatiwa namba ya usajili baada ya kukamilisha malipo husika.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 2020 hadi kufikia Julai 2023 wastani wa mapato ya Serikali yaliyokusanywa kwa mwaka kutokana na usajili wa vyombo vya moto ni Sh2.071 bilioni,” amesema.

Related Posts