Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema ili kufika malengo ya ajenda ya 2063 ya nchi wanachama wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), mataifa hayo hayana budi kuboresha miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege kurahisha usafiri na usafirishaji wa biashara.
Hemed amesema hayo Juni 25, 2024 alipofungua mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wa Biashara AfCFTA, Unguja.
Amesema Afrika pia inakabiliwa na changamoto ya usalama, nishati, barabara, usafiri wa anga, uzalishaji mdogo, na mawasiliano hafifu.
“Ili kufika malengo yetu tunatakiwa kujikita katika maeneo mbalimbali, hususani tuboreshe miundombnu ya barabara, bandari, na viwanja vya ndege ili kurahisha biashara na kuwezesha biashara ndogondogo ziweze kushiriki katika ngazi ya kikanda na kimataifa, kuhakikisha upatikanaji wa mikopo, na kutoa elimu ya masoko kwa wajasiriamali wetu,” amesema.
Hemed amezitaka nchi husika kupitia mawaziri wa biashara kuhakikisha maeneo ambayo ni huru kushirikiana na mataifa jirani ili sera za kiuchumi na kibiashara ziendane.
Jambo jingine amesema ni kuboresha mazingira ya uwekezaji, kupunguza urasimu, kuimarisha utawala bora, na kuhakisha usalama wa wawekezaji na mali zao, ili kuvutia wawekezaji.
Amesema mataifa hayo yanapaswa kujenga uwezo wa watu, kwani maendeleo ya uhakikia hayawezi kupatikana bila uwezo, kwa hiyo wanao wajibu wa kuwekeza katika elimu na afya ili kupata watu wenye uwezo wa kushindana kimataifa.
“Wakati hayo yakifanyika ni muhimu kuzingatia masuala ya kijamii kwani uchumi unatakiwa kwenda sambamba na utunzaji wa mazingira, elimu ya afya na mafunzo ya ufundi ili kuhakikisha tunakuwa na nguvu kazi yenye ujuzi kushindana,” amesema.
Amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na nchi zote wanachama wa AfCFTA katika kufanikisha malengo hayo.
Amezipongeza nchi ambazo zimeanza kufanya biashara ya ndani ya Afrika kwa kutumia cheti cha uasili wa bidhaa cha eneo huru la biashara, akisema Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo ambazo zimepiga hatua.
“Katika kutumia cheti cha uasili wa bidhaa cha eneo huru wa Afrika, Tanzania imechukua hatua za kuelimisha na kujenga uwezo wa sekta binafsi ili wachangamkie fursa na juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda. Kuna kampuni 11 zinazofanya biashara kwa kutumia cheti cha uasili,” amesema.
Kwa mujibu wa Hemed, eneo huru la bishara linaweza kuwa chachu ya maendeleo ikiwa wataweka nguvu katika uwekezaji.
Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA, Wamkele Mene amesema wanaweka mifumo mizuri ya kisheria kusaidia ukuaji wa biashara.
Amesema chini ya viongozi wakuu wa nchi hizo na mabaraza ya mawaziri wamefanya mengi lakini bado kuna mambo ya kufanya kufikia malengo.
“Kuna biashara za huduma, za kidijitali na zote hizi zitakazofanyika lazima ziheshimu makubaliano ya AfCFTA, na tutaendelea kufanya kazi na wabia wetu ili kuhakikisha biashara inakuwa mara mbili kadri tunavyoendelea,” amesema.
Mwakilishi wa shirika la eneo huria duniani, Dk Samir Hamrouni amesema eneo huru ni msingi imara wa maendeleo katika uchumi, kisiasa na kiutamaduni.
Amesema litasaidia kujitegemea na kuwa na maamuzi na nguvu ya pamoja.
“Tumeona jukumu linakwenda kuvutia wawekezaji na kusonga mbele katika viwanda, tunaona kanda takribani 200 kuna miradi 73 katika nchi 47 kati ya 52 za Afrika,” amesema.
Hata hivyo, amesema kuna haja ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ufanyaji biashara kwa nchi wanachama.
“Tunahitaji ushirikiano na kujifunza baina ya nchi na nchi kutekeleza miradi ili kufika mbali katika mapinduzi ya viwanda,” amesema.
Awali, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban amesema mkutano huo ulioanza Juni 18, unaweka misingi imara ya utekelezaji thabiti wa mipango ya AfCFTA
Shaaban ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la AfCFTA amesema wamejadiliana kuangalia biashara na mapinduzi ya viwanda kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa.
“Tumezungumzia fursa zilizopo, eneo mojawapo ni uzalishaji wa vipuli vya magari, hivyo nchi wanachama zinatakiwa kuchangamkia fursa,” amesema.
Amesema wamegundua uwepo wa changamoto za ufanyaji biashara ikiwemo miundombinu ya uzalishaji duni, nishati na gharama za mawasiliano.
“Tanzania imeanza kuzifanyia utatuzi, ikiwemo kujenga reli ya kisasa ya SGR na kujenga kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere, miundombinu hii ikikamilika itaimarisha biashara,” amesema.