Dar es Salaam. Ni faraja katika mapambano ya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU), baada ya watafiti kupata chanjo ya kinga kupitia dawa ya PrEP iliyo katika mfumo wa sindano.
Utafiti uliofanywa kwa wasichana 2,134 nchini Uganda na Afrika Kusini ulibaini hakuna maambukizi ya VVU yaliyoonekana katika jaribio la msingi la PrEP ya sindano, ambayo walidungwa kila baada ya miezi sita.
Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) bado halijaeleza chochote kuhusu chanjo hiyo.
Kwa zaidi ya miaka mitano Tanzania imekuwa ikitumia dawa kinga aina ya PrEP, iliyo katika mfumo wa vidonge vya kumeza kila siku kujikinga na maambukizi mapya ya VVU ambayo ilizua changamoto kwa wenza na unyanyapaa.
Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Gilead Sciences ulitolewa Alhamisi Juni 20, 2024 na kuchapishwa katika tovuti ya New York Times na CNBS, za Marekani ikielezwa umekuwa na mafanikio zaidi katika ngazi ya mwisho.
“Ni nadra kwa taasisi yoyote ya kisayansi katika majaribio ya dawa mpya kupata ufanisi wa asilimia 100, lakini ndivyo ilivyotokea wiki iliyopita, wakati Taasisi ya Gilead Sciences ilipotangaza kwamba hakuna maambukizi ya VVU ambayo yameonekana kati ya wasichana 2,134 nchini Afrika Kusini na Uganda.”
“Waliochomwa sindano mara mbili kwa mwaka za dawa ya kupambana na VVU ya lenacapavir ambayo ni mfumo PrEP hawakupata maambukizi,” ilisema tovuti ya Aids Map iliyojikita kutoa habari kuhusu VVU na Ukimwi.
Utafiti huo ulihusisha wasichana wenye umri wa kati ya miaka 16-25 katika maeneo 25 nchini Afrika Kusini na maeneo matatu ya Uganda.
Mkurugenzi wa Kituo cha VVU cha Desmond Tutu katika Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini, Linda-Gail Bekker amesema kupatikana kwa chanjo hiyo ni mafanikio katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kutapunguza unyanyapaa.
“Ingawa tunajua njia za kitaalamu za kuzuia VVU ni nzuri zinapochukuliwa kama ilivyoagizwa, lakini sindano hizi zinaweza kusaidia kukabiliana na unyanyapaa na ubaguzi ambao baadhi ya watu wanaweza kukabiliana nao wakati wa kuchukua au kuhifadhi dozi za PrEP, pia ni hatua nzuri dhidi ya mapambano dhidi ya VVU,” amesema.
Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya MDH iliyopo nchini Tanzania, Dk David Sando amesema wamekuwa wakishirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kusambaza dawa kinga za vidonge aina ya PrEP.
Amesema kwa sasa duniani kumekuwa na maendeleo, mtu anaweza kupata kinga kwa njia ya sindano na kukaa muda mrefu, ambalo ni suluhisho zuri tofauti na vidonge vya kumeza kila siku.
Hata hivyo, Sando alisema pamoja na faida ya kukaa muda mrefu bila kumeza tembe, bado jamii inahitaji uelewa na elimu ya kutosha kuhusu sindano hizo, ambazo alisema pia zinahitaji uchunguzi wa kina kujiridhisha.
“Naamini Serikali ipo kwenye mchakato wa kujifunza na kuona kama sindano itakuwa na manufaa zaidi, dawa ya sindano hubaki mwilini kwa muda mrefu hivyo inaweza kuwa na madhara madogo madogo,” amesema.
“Ile haiondoki ndani ya damu kwa muda mfupi, ikiisha miezi sita inabaki kwa kiwango kidogo, hivyo mtu asipotumia tena sindano na akaendelea bila kinga kuna uwezekano akapata maambukizi na virusi vikajenga usugu na ile dawa kiasi kwamba vinaweza kuja kwa aliyepata chanjo ndani ya muda vikamfikia upya, tatizo la usugu likaingia hapo,” amesema Sando.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Taifa wa wanawake wanaoishi na VVU Tanzania (NNW+) Veronica Lyimo amesema kimatumizi sindano ni rahisi zaidi kuliko kutumia dawa za kila siku.
Amesema sindano inampa mtu uhuru, anakaa baada ya miezi kadhaa hakuna atakayejua kuwa alichoma sindano, kwani kutembea na dawa wasiozijua ARV na kinga za PrEp wanajua anatumia ARV ilhali mtu anatumia dawa kinga.
“Vindonge vinaleta unyanyapaa, sindano ikija itampa mtu uhuru wa kuchagua, kuna utafiti mdogo tulifanya na Shirika la Vijana kujua mapendekezo na maoni ya wadau na hayo ndiyo maoni waliyatoa,” amesema.
Veronica amesema hata makopo wanayotumia kuwekea dawa za ARV na PrEP utofauti wake ni kwenye rangi pekee, lakini ukiangalia kwa mtu ambaye siyo mwelewa atahisi mtu anameza ARV. Zikiwa ndani ya kopo kama kwenye pochi zinalia mara kwa mara,” alisema.
Mbali na utafiti huo, Taasisi ya Gilead Sciences kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita iligundua vidonge vya PrEP ambavyo viliidhinishwa kutumiwa na watu wasio na VVU lakini wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi.
Hii si mara ya kwanza kwa chanjo au tiba ya ugonjwa huo.
Majaribio kwa binadamu yaliwahi kufanyika Agosti 2019 ya chanjo ya VVU iliyokuwa inafanyiwa utafiti kwa muda mrefu na Kampuni ya Moderna ya Marekani.
Chanjo hizo zilipewa jina la mRNA-1644 na mRNA-1644v2-Core, ambazo zilichunguzwa na kufanyiwa majaribio ya awali na kuonekana salama kabla ya kujaribiwa kwa binadamu kwa mara ya kwanza.
Wanasayansi na watafiti wa dawa kinga hiyo, Pre-Exposure Prophylaxis (PrEP) wanasema inaweza kuzuia maambukizi ya VVU ikiwa mtumiaji atameza kila siku kwa muda wa siku saba kabla ya kujamiiana.
Dawa hizo za tembe zenye uwezo wa kukinga maambukizi dhidi ya VVU kwa asilimia 99 zilianza kutumika katika baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika mwishoni mwa 2010.
Utafiti uliofanywa na mwanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha London, Dk Sheena McCormack ulionyesha PrEP inazuia maambukizi ya VVU kwa kuua virusi baada ya kufanyiwa majaribio kwa kundi la wapenzi wa jinsia moja, ambao wamo katika hatari zaidi ya kuambukizwa.
Mwanaharakati wa kupambana na VVU/Ukimwi kutoka Shirika la AVAC la Marekani, Kennedy Mupeli amesema mhusika anatakiwa kusubiri kwa siku saba baada ya kumeza tembe ili dawa ifanye kazi sawasawa.
Amesema baada ya muda huo atakuwa salama kufanya tendo hilo na atatakiwa kuendelea bila kuacha, isipokuwa atakapoona hayupo kwenye vihatarishi vya kupata maambukizi.
“Lazima mtu ahakikishe anatumia kwa usahihi bila kukosa na kupata ushauri kwa mtaalamu wa afya pindi atakapohitaji kuacha kutumia PrEP,” amesema Mupeli.
Akizungumzia walengwa wa dawa hizo, Dk Sheena amesema PrEP ni kwa ajili ya ambao bado hawajaambukizwa VVU na inapendekezwa kutumiwa na watu ambao wapo katika hatari zaidi ya kuambukizwa.