Mambo manne yaliyowakuta Jesca, Egina Afrika Kusini

WIKIENDI iliyopita mabondia Jesca Mfinanga na Egine  Kayange walikuwa na vibarua vya mapambano ya kimataifa nchini Afrika Kusini ambayo yalifanyika katika jiji la Johannesburg.

Katika mapambano hayo, Jesca alikuwa na kibarua  cha kuwania mkanda wa Ubingwa wa Afrika ‘ABU’ katika uzani wa fly dhidi ya Simangele Hadebe wa Afrika Kusini, pambano la raundi kumi wakati Egine Kayange alikuwa na pambano la kuwania mkanda wa Afrika ‘ABU Sadc’ kwa nchini za Kusini mwa Afrika dhidi ya Monica Mukandla kutoka Zimbabwe, pambano la raundi kumi uzani wa bantam.

Lakini mabondia hao wamekutana na vipengele vizito hali ambayo imepelekea wakwame nchini humo hadi kufikia jana mchana walikuwa hawana dalili yoyote ya kuweza kutoka.

Katika hali ya kushangaza pambano kati ya Jesca Mfinanga na Simangele Hadebe lilimalizika kwa utata wa matokeo yaliotokea baada ya mwamuzi wa pambano hilo kulimaliza kimaajabu hali iliopelekea sintofahamu upande wa Jesca.

Pambano hilo ambalo lilifanyika juzi na kupelekea mzozo mkubwa upande wa Mtanzania huyo hali iliyolazimu kulalamikia matokeo hayo kwa waandaji wa pambano hilo ambao waliwapa ahadi ya matokeo yake kutoingizwa kwenye mtandao wa boxrec.

“Mwamuzi sijui ilikuwaje akawa amekata pambano maana mpinzani ndiyo alikuwa ameumia ila ajabu ndiyo wamemtangaza kuwa mshindi, tumeongea na promota na bado vikao vinaendelea kwamba matokeo yasiwekwe kwenye rekodi za boxrec,” alisema Jesca kwa njia ya simu.

Hata hivyo Mwanaspoti lilimtafuta Rais wa ABU,  Houcine Houchi raia wa Tunisia ambaye alianza kwa kutumiwa video ya pambano na mwandishi wetu kabla ya kuulizwa juu ya uhalali wa matokeo hayo ambapo alisema kuwa:

“Hapana kukuwa na ajabu kwa mujibu wa msimamizi wa pambano kuwa mpinzani (Jesca)  alikuwa anakimbia nje ndiyo maana Semangele amepewa ushindi,” alisema Houchi lakini baada ya muda alituma jumbe mwingine akiomba kusubiri ripoti ya mwamuzi na msimamizi wa pambano kisha atatoa majibu yake kabla ya juzi Jumatatu kuulizwa tena na majibu yake yalikuwa hivi:

“Najua kama mwandishi wa habari unapenda kuandika habari nzuri, lakini, bado tunangojea ripoti hizi mbili na hakuna malalamiko kutoka kwa timu ya Jessica yaliyopokelewa hwa hivyo, tafadhali kuwa na subira na ikiwa kuna habari yoyote nitakuambia.

Hata hivyo Mwanaspoti lilimtafuta bondia mkongwe na mwamuzi wa ngumi za kulipwa nchini, Emmanueli Mlundwa ambaye alisema kuwa ni jambo gumu kwake kutoa maoni ya moja kwa moja ya maamuzi ya pambano hilo kwa kuwa mwamuzi ndiyo alikuwa anaona kilichotokea ingawa kwa upande wake ameona kitendo cha Jesca kumkimbia mpinzani wake kimempa sababu za mwamuzi kumaliza pambano hilo.

Kwa upande wa Egine yeye pambano lake na Monica lilishia raundi ya nne baada ya raia wa Afrika Kusini kujichomeka katika kona yake na kurusha taulo kuashiria ameshindwa kuendelea na pambano hivyo ikawa amepigwa kwa TKO.

Mabondia hao walikuwa wakitarajia kurejesha nchini juzi Jumatatu kwa ndege ya mchana lakini kutokana na promota wa pambano lao kushindwa kuwalipa kwa wakati wakajikuta wameachwa na ndege.

“Inshu pesa atujapewa hadi sasa na mda wa ndege tayari umeshapita na hotelini  tumetolewa  leo hotelini (juzi),  gharama zinazidi, tumeletwa kwa mtu binafsi ambaye ni jamaa aliyetufuata  ‘airport’ tulivyofika ndiyo tupo kwake na yeye  hadi sasa hajarudi aliwapeleka mabondia wa Limpopo Airport baada ya sisi kugoma katuacha hapa bado  hajarudi”, alisema Jesca.

Mabondia hao kwa sasa bado wapo Afrika Kusini baada ya kugomea kurejea nchini hadi pale watakavyolipwa pesa zao.

Mwanaspoti limemtafuta wakala aliyesafiri na mabondia hao, Innocent Everist ambaye amedai kuwa hawezi kukubali kuondoka hadi mabondia hao watakapolipwa.

“Sasa hivi kuna sehemu ndiyo tupo tumekaa na promota ameshatueleza anaweza kutulipa kesho kisha atatukatia tena tiketi za ndege kwa ajili ya kurudi.

“Kuhusu matokeo ya pambano la Jesca tutashughulikia ingawa kwa sasa tunapambana pesa ipatikane ili mambo mengine yaweze kukaa sawa,” alisema Evarist ambaye pia ni bondia.

Wakati wao wakiendelea kusubiri pesa zao ambazo zimekwama na kuwafanya washindwe kutoka Afrika Kusini lakini msimamizi wa pambano hilo, Lehlohonolo Ramagole  hadi kufikia jana mchana alikuwa ameshaweka matokeo ya mapambano yote  katika mtandao wa boxrec  yakionyesha Jesca Mfinanga amepigwa kwa TKO ya raundi ya kwanza kama Egine Kayange aliyepigwa kwa TKO ya raundi ya nne.

Related Posts