Kanuni mikopo ya asilimia 10, kukamilika Juni 30

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema maandalizi ya kanuni za utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu nchini yatakamilika Juni 30, 2024.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Juni 26, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoana Serikali za Mitaa, (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa wakati akijibu hoja za wabunge zilizochangiwa katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25.

Mchengerwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini kurudishwa, baada ya kusitishwa mwaka 2023.

Amesema pia ameshauri namna nzuri ya kuitoa, ili kuongeza wigo kwa wanaopata mikopo hiyo.

“Naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu na Watanzania ifikapo Juni 30, 2024 maandalizi ya kanuni za utolewaji wa mikopo yatakuwa yamekamilika na ifikapo Julai 10, 2024 watalaamu watafika katika kila jimbo kutoa mafunzo na elimu ya utoleaji wa mikopo hiyo,” amesema.

Amesema fedha za kutosha zipo za utoaji wa mikopo hiyo na kwamba wana bakio la zaidi ya Sh307 bilioni.

Amesema katika makusanyo ya mwaka 2024/25 ni matarajio yao kutoa mikopo yenye thamani ya Sh101.5 bilioni.

Amezitaja halmashauri 10 zitakazoanza kutoa mikopo hiyo ni halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dodoma, Songea, Kigoma Ujiji, Mbulu, Newala Halmashauri ya Wilaya ya Kitilima, Nkasi, Bumbuli na Siha.

Amesema halmashauri 174 zitapata mikopo kwa utaratibu ulioboreshwa zaidi na kwamba dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan fedha hizo ziwafikie.

Aprili 13, 2023, akihitimisha hoja ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2023/24, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kusitishwa kwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri hadi hapo utaratibu mwingine utakapoelezwa.

Hatua hiyo ilitokana na malalamiko ya namna zinavyokopeshwa na urejeshaji, ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Related Posts