VITENDO vya ubakaji, mauaji yatokanayo na visa vya wivu wa mapenzi na imani za kishirikina, vimetajwa kuwa ni moja ya changanoto zinazoikumba jamii hali inayosababisha kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili. Anaripoti Ibrahim Yassin … Songwe, (endelea).
Kauli hiyo imetolewa jana Jumanne na Mkuu wa wilaya ya Songwe, Solomoni Itunda katika hitimisho la mkutano wa injili uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Ichenjezwa wilayani Mbozi.
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, Itunda amesema viongozi wa nyumba za Ibada na waumini wengine wana nafasi kubwa kukemea vitendo hivyo wakiwa kwenye mikutano ama madhabahuni ili jamii iishi kwa kumtegemea Mungu.
Mkutano huo ulioendeshwa na uongozi wa kanisa la New Life in Christ ambayo ni muungano wa makanisa mbalimbali ya kikristo nchini, umefanyika kwa muda wa siku saba mkoani Songwe.
Akiwasilisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan, Itunda ameeleza kuwa Rais Samia anatambua kazi inayofanywa na viongozi wa dini ndiyo maana amekuwa akishirikiana nao katika mambo mbalimbali.