WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima,akizungumza wakati akizindua Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) lililozinduliwa leo Juni 26,2024 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima,akifafanua jambo wakati akizindua Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) lililozinduliwa leo Juni 26,2024 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) lililozinduliwa leo Juni 26,2024 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima,ametoa wito kwa Viongozi na Wajumbe wote wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo wa hali ya juu.
Waziri Gwajima ametoa wito huo leo Juni 26,2024 wakati akizindua Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) jijini Dodoma.
Waziri Gwajima amewapongeza Viongozi wote 30 wa Baraza hilo waliochaguliwa kwa kuaminiwa na Wajumbe katika Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania Bara na Makundi Maalum.
“Sasa mmechaguliwa na kuaminiwa nendeni mkafanye kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo ili kukidhi matarajio ya waliowachagua na jamii ya Watanzania kwa ujumla.”amesema Waziri Gwajima
Viongozi hao waliochagulia ni Ndugu Japser Lazaro Makala Mwenyekiti wa Baraza, Ndugu Adamson Richard Nsimba – Katibu Mkuu wa Baraza, Ndugu Prisca Matiwili – Mweka Hazina wa Baraza, Mwenyeviti wa Kamati mbalimbali, pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
“Nimepokea kwa mikono miwili taarifa ya Kamati ya Mpito. Katika taarifa hiyo, nimesikia mapendekezo ya Kamati ambayo mengine utekelezaji wake unahitaji kujitoa kwenu kwa hali na mali, lakini mengine ni ya kwetu upande wa Wizara.”amesema
Aidha amesema kuwa Masuala ya uwakilishi wa kikanda, upatikanaji wa rasilimali fedha na mapitio ya Kanuni za Uchaguzi wa Baraza, ni masuala ambayo mnaweza kuyajadili kupitia mifumo yenu ya ndani na kuchukua hatua, lakini kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayoratibu shughuli za Baraza.
Waziri Gwajima amesema kuwa tayari walishaanza mchakato wa kutoa mafunzo kwa Wasajili Wasadizi na zoezi hilo ni endelevu.
Aidha, kuhusu kuwajengea uwezo Wajumbe wapya wa Baraza, amewahakikishia kuwa suala hilo lipo ndani ya uwezo wao na milango ya Wizara iko wazi wakati wowote.
Hata hivyo ameishukuru Kamati ya Mpito kwa kuratibu Uchaguzi huo kwa weledi, viongozi na Wajumbe wote wa Baraza kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kuliongoza Baraza kwa kipindi cha miaka mitatu . Naomba mfanyia kazi marekebisho ya Kanuni za Uendeshaji na Uchaguzi wa Baraza.
“Nendeni mkatekeleza agizo la Serikali la kuzifanyia marekebisho kanuni za uendeshaji na uchaguzi ili uchaguzi ujao usimamiwe na mifumo ya NaCoNGO badala ya kuendeshwa chini ya bodi ya uratibu wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali”amesisitiza
Kwa upande wake Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’S) Bi.Vickness Mayao,ametoa wito kwa NaCoNGO kutumia nafasi yao kuishauri Serikali kwenye masuala ambayo wanaona kwamba yanajenga kwani mashirika yasiyo ya Kiserikali yanafanya kazi katika Sekta zote.
“Wao wakiweza kujiratibu wenyewe na kuangalia mapungufu yaliyopo na kuishauri Serikali vizuri kuhusiana na changamoto mbalimbali ambazo inapaswa kuzichukua na kuzifanyia kazi”,amesema Mayao
Naye Mwenyekiti Mpya wa NaCoNGO Bw.Japser Lazaro Makala,amesema wamejipanga kuanza kazi mara baada ya Baraza kuzinduliwa ambapo watakuwa na vikao vya kujadili namna ambavyo watajipanga kufanya kazi ikiwemo kuandaa mpango kazi mzuri.
“Kwasababu sisi ni baraza la Taifa pia tupo huru tutaishauri Serikali tuweze kutengeneza kikosi kazi ambapo kitakuwa kinaratibu zoezi zima la kupata kanuni mpya za Baraza la mashirika yasiyo ya Kiserikali “,amesema Bw.Makala