Geneva, Uswisi. Katika hali ya kusikitisha inaelezwa watoto 10 kwa siku wanapoteza mguu mmoja au yote wawili katika vita vinavyoendelea kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas, huko Gaza.
Akitoa ripoti hiyo, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosaidia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) Philippe Lazzarini, amesema kwa takwimu hizo karibuni watoto 2,000 wamepoteza miguu tangu kuanza kwa vita hivyo ambazo ni zaidi ya siku 260.
“Kimsingi tuna kila siku watoto kumi ambao wanapoteza mguu mmoja au miguu miwili kwa wastani. Kumi kwa siku, hiyo ina maana karibu watoto 2,000 baada ya zaidi ya siku 260 za vita hivi vya kikatili,” amesema Lazzarini huko Geneva.
Akinukuu takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), amesema takwimu hiyo haijumuishi mikono, bali ni miguu pekee huku akiongeza kwamba wana takwimu nyingi zaidi.
Amesema zoezi la kuwakata viungo watoto hao mara nyingi hufanyika katika hali mbaya wakati mwingine bila ganzi. Mbali na mashambulizi ya Israel, njaa na upungufu wa maji mwilini pia husababisha madhara kwa watoto hao.
Kwa mujibu wa tovuti ya Morocco World News, maofisa wa Gaza wamesema takribani watoto 40 wa Kipalestina wamekufa katika eneo lililozingirwa kutokana na utapiamlo, huku kukiwa na uhaba wa chakula, maji na vifaa vya matibabu.
Daktari Kamal Safiyya, Mkuu wa Hospitali ya Kamal Adwan ilyopo Kaskazini mwa Gaza, ameiambia Al Jazeera kwamba watoto wengi hufa kutokana na lishe duni huku akiongeza, “Tumeandika matukio mengi ambapo watoto walikuwa na utapiamlo mkali.”
Katika suala hilo, Mkuu wa UNRWA ameangazia kupeleka misaada kwenye ukanda huo uliokumbwa na vita inayokaribia mwaka sasa.
Aidha, Shirika la Save the Children limesema watoto 21,000 wanakadiriwa kupotea katika machafuko ya vita hivyo, Shirika la Habari la AFP limeandika.
Hata hivyo, Wizara ya Afya ya Gaza imesema takribani watu 37,658 wameuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel kutokana na shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023 kusini mwa Israel.
Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 1,195, wengi wao wakiwa raia, kulingana na takwimu rasmi za Israeli. Aidha Hamas walichukua watu 251 mateka katika shambulio hilo, 116 kati yao wakisalia mateka katika Ukanda wa Gaza, kulingana na Israel huku ikielezwa kuwa 42 kati yao wamekufa.