LHRC yadai bajeti ya 2024/25 haijagusa maendeleo ya wananchi

Dar es Salaam. Wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano likipitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema haijagusa maisha ya wananchi.

LHRC imesema bajeti hiyo imejikita zaidi kwenye matumizi ya kawaida kuliko miradi ya maendeleo, huku ikitoa mapendekezo ambayo wanaamini yakifanyiwa kazi itakuwa nafuu kwa wananchi.

Katika bajeti hiyo, Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh49.35 trilioni ambayo ni ongezeko la asilimia 11.2 kulinganisha na bajeti ya mwaka 2023/2024.

Hata hivyo, akitoa taarifa ya hali ya uchumi bungeni Dodoma leo Juni 26,2024, Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema kipaumbele cha Serikali ni kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi, ili uchumi huo upunguze umaskini na kuwawezesha wananchi kuzalisha.

“Ili tufike kwenye eneo hilo, lazima tufike kwenye ekta zinazobeba watu wengu… sekta ya kwanza ni ya kilimo kwa sababu inabeba asilimia 65 ya watu wetu na inachukua zaidi ya robo ya pato la Taifa,” amesema.

Ametaja maeneo mengine kuwa ni pamoja na viwanda, biashara na usafirishaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akihitimisha mjadala wa bajeti hiyo, amesema Serikali imesikiliza hoja za wabunge na itabana matumizi, ili kufidia fedha ambazo imeshazipangia kwenye wizara za kisekta na kuhakikisha shughuli za kisekta hazikwami.

“Nimemwelekeza mlipaji wa Serikali kwenye Sh129 bilioni zilizowekwa kwa ajili ya kununua magari, akate zaidi ya asilimia 50, abakize Sh50 bilioni tu, wapeleke kwenye maeneo muhimu.

“Hivyo hivyo kulikuwa na Sh67 bilioni za matengenezo, akate kwa asilimia 50, hivyo hivyo kwenye mafuta akate asilimia 50. Fedha hizo zitakweda wenye miradi ya maendeleo ambayo itaathirika na marekebisho ya sheria ya fedha,” amesema.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 26, 2024 Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Fulgence Massawe amesema bajeti hiyo imejikita kwenye matumizi ya kawaida ya Serikali kwa asilimia kubwa ambayo hayamgusi mwananchi wa kawaida.

“Asilimia 70 ya bajeti hii ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo hayajamgusa mwananchi, asilimia 30 ndiyo imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo. Hii inaonyesha tusitegemee maendeleo makubwa au miradi mipya kwa kuwa bajeti yetu ni ya matumizi ya kawaida, imejikita pia kwenye kulipana mishahara na madeni,” amesema.

Ameyataja matumizi hayo kuwa ni pamoja na magari ya kifahari, watendaji wakuu wa nchi kuishi Dar es Salaam muda mwingi kuliko Dodoma, hivyo kusababisha Serikali kuingia gharama mara mbili.

Kiongozi huyo wa LHRC amekwenda mbali zaidi na kubainisha kwamba kuna haja ukubwa wa Serikali kuangaliwa upya, akitolea mfano kuongeza cheo cha Naibu Waziri Mkuu na wizara kuwa na waziri, naibu waziri, katibu mkuu na naibu katibu mkuu.

“Wizara ni nyingi na kuwa na viongozi wote hao kunaongeza gharama na tukiangalia bajeti yetu mara nyingi imekuwa na nakisi ambayo huwa haiathiri matumizi ya kawaida zaidi ya miradi ya maendeleo,” amesema.

Changamoto nyingine ambayo LHRC imeitaja ni kushindwa kubuni vyanzo vipya vya mapato, matumizi ya fedha za kigeni na deni la Serikali.

“Deni limeendelea kuongezeka na kufikia Sh91.7 trilioni Machi, 2024 ukilinganisha na la mwaka 2022 Sh 69.44 trilioni.

“Hii inaashiria kwamba ugumu wa maisha unaweza kuongezeka ukisababishwa na kulipwa kwa deni hilo.

“Tunashauri Serikali ipunguze gharama za uendeshaji, ikiwamo posho, maisha na magari ya kifahari ambavyo vinaweza kuwa na mbadala,” amesema.

Akiendelea kuchambua mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2024/2025 yaliyowasilishwa Bungeni Juni 13 mwaka huu na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, Massawe amesema pia bajeti inakinzana na jitihada za kimataifa za kutunza mazingira.

Amesema kuweka tozo kwenye gesi inayotumika kuendesha mitambo kama vile injini za magari na bajaji pamoja na kuweka kodi kwenye magari ya umeme, pendekezo hilo la Serikali linarudisha nyuma lengo namba 13 la malengo endelevu ya dunia.

Pia LHRC imependekeza kuwepo na uwajibikaji na uwazi kwenye ukusanyaji na utumiaji wa fedha za bima ya afya kwa wote, huku ikionyesha wasiwasi kwenye kikokotoo cha malipo ya pensheni ambacho waziri alisema pendekezo ni la muda mfupi.

Related Posts