Yanga yaruhusiwa kusajili baada ya kumlipa Kambole

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), limeindolea Klabu ya Yanga zuio la kusajili wachezaji.

Yanga ilikumbana na rungu la kufungiwa na FIFA ikikabiliwa na kesi mbili, baada ya kufanya makosa ya kwenye mfumo wa usajili kwa kushindwa kukamilisha taarifa muhimu za mmoja wa wachezaji wake wa zamani kabla ya kuweka sawa na kuondolewa adhabu hiyo.

Kesi ya pili juu ya kutomlipa aliyekuwa mchezaji wao Lazarous Kambole ambaye ilimsitishia mkataba bila kumlipa ujira wake.

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jioni hii imesema FIFA imeiondolea Yanga adhabu hiyo baada ya kumalizana na Kambole kufuatia kushindwa kumalizana ndani ya siku 45 tangu hukumu hiyo ilipotoka.

Awali Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema tayari walishamalizana na Kambole lakini kilichokuwa kinasubiriwa na FIFA ni kujiridhisha kama malipo hayo yamemfikia Mzambia huyo.

Kufunguliwa kwa Yanga kunaiweka huru timu hiyo kushusha majembe mapya kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa.

Yanga inatajwa tayari imeshamalizana na kipa Khomeiny Aboubakar kutoka Singida Black Stars, beki Chadrack Boka (FC Lupopo), kiungo Clatous Chama (Simba) na mshambuliaji Prince Dube (Azam).

Hivi karibuni, Kamwe alisema timu yao itaanza kutambulisha wachezaji itakaowaacha na wale watakaoingia kuanzia Julai Mosi mwaka huu.

Related Posts