Mbezi Msumi waanza kuchimbiwa visima

Dar es Salaam. Hatimaye wakazi wa Mtaa wa Mbezi Msumi wilayani Ubungo, Dar es Salaam wameanza kuchimbiwa visima vya maji, ili kutatua kero hiyo, wakati wakisubiri mradi mkubwa wa maji wa Sh18 bilioni.

Awali, Juni 20, 2024 wakazi wa mtaa huo walipinga uchimbaji wa visima hivyo, baada ya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew kutembele eneo hilo ambalo halina mradi wa maji ya bomba yanayotolewa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Dawasa).

Wananchi hao ambao baadhi yao walibeba mabango yenye ujumbe wa kudai maji, walisema kama ni visima tayari wanavyo na kwamba wako tayari kusubiri mradi wa maji wa Sh18 bilioni.

Hatua ya Naibu Waziri Mathew kutembelea eneo hilo, ilitokana na gazeti la Mwananchi kuripoti kuwa wananchi hao wanatumia maji ya vijito na kuyasafisha kwa kutumia saruji, ili yafae kwa matumizi ya nyumbani.

Akizungumza na wananchi hao, Mhandisi Kundo alisema pamoja na dhamira ya Serikali kutenga fedha za mradi mkubwa maji, mradi huo utachelewa zaidi ya mwaka, hivyo watawachimbia visima ili wapate maji kwa muda wanaosubiria mradi huo.

Kauli hiyo ilipingwa na baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye mkutano wa naibu waziri huyo wakisema hawahitaji visima.

Leo Juni 26, 2024 Mwananchi imeshuhudia visima hivyo vikichimbwa, baada ya Dawasa kutembelea eneo hilo na baadhi ya wananchi waliozungumza wamesema wamevikubali.

Everlasting Lyaro, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano Dawasa, amesema visima hivyo vinavyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji Visima (DDCA) vina urefu kuanzia mita 170 kwenda chini.

“Urefu huu unakwenda hadi chini kwenye matabaka ya maji safi, mengi na yenye ubora tofauti na visima vya wakazi wa hapa vyenye mita kuanzia 80 hadi 100 ambavyo viko katika miamba yenye maji ya chumvi nyingi.

“Vitatumia wiki mbili kukamilika na kuanza kutoa huduma katika mitaa ya Msumi A, B na C na vitawanufaisha wakazi zaidi ya 140,000,” amebainisha.

Amesema eneo hilo limekosa miundombinu ya Dawasa kwa kipindi kirefu, hivyo wakazi hao wamekosa huduma ya maji hadi Serikali ilipokuja na mpango wa uchimbaji visima hivyo vitatu, kisha ujenzi wa mradi mkubwa wa Sh18 bilioni.

“Baada ya kukamilika zitaanza kujengwa vituo vya usambazaji katika mitaa ya hapa kwa hiyo wakazi watapata maji bora.”

Akizungumza leo baada ya hatua ya kuanza kuchimba kwa visima hivyo, Francis Kiwanga, mkazi wa mtaa huo amesema wameteseka vya kutosha na sasa hatua hiyo itawaokoa kupata maji bora.

“Ni kweli tuligoma alipokuja naibu waziri, lakini tukahamasishana tukubali baada ya kupata elimu kuwa visima hivi ni virefu tofauti na vyetu, hivyo maji yake ni mazuri na gharama nafuu,” amesema Kiwanga.

“Tunachoomba yatoke tu maji mazuri na bora, huku mtaani tunanunua ndoo moja Sh200, lakini tunaambiwa huku tumewahamasishna na wenzetu walio wengi wameomba wapate maji mazuri,” amesema Kiwanga.

Kwa upande wake, Nasma Abubakar amesema wamekuwa wakitumia muda na umbali mrefu kufuata maji.

“Nimekuwa nikiamka saa 10 alfajiri kila siku kutafuta maji, huwa nachoka na yanauzwa bei ya juu. Nashukuru kwa hatua hii itanisaidia kama mama wa familia,” amesema.

Antony Milomuyawantu, amesema ni kweli mwanzo wananchi walionyesha shaka kutokana na ahadi hewa, ila wameridhia na wanachotaka ni maji ya kunywa.

Awali Juni 20, 2024 baadhi ya wananchi waliozungumza katika mkutano wa Naibu Waziri Mathew walitaka kuhakikishiwa kama maji hayo yatakuwa na chumvu au la, huku wengine wakisema visima hivyo havina tofauti na walivyonavyo ambavyo hutoa maji ya chumvi.

Akizungumza baada ya kupewa nafasi, Desideria Diradina alisema wako tayari kusubiri mradi huo kuliko kuchimbiwa visima.

“Maji ya chumvi tayari tunayo,” alisema.

Naye Joseph Kaduma alisema, “Kinachotusikitisha tunaambiwa kwamba huduma itapatikana labda baada ya mwaka mmoja, halafu mtuongezee visima.

“Kuna watu walijiongeza wakachimba visima, tunalipa Sh4,000 kwa uniti moja, sasa mnataka mlete jinamizi ligine la kuchimbiwa visima, utakuwa ni mzigo mzito,” alisema.

Alisema kwa kuwa bomba la Dawasa lipo kilometa 10 kutoka Msumi, wavutiwe maji haraka.

“Leo tunaambiwa tujegewe visima, litakuwa ni jinamizi kubwa,” alisema.

Related Posts