Nairobi. Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amemtaka Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa hilo, Noordin Haji ajiuzulu kutokana na kushindwa kumshauri Rais William Ruto vizuri kuhusu sakata la maandamano ya Gen Z.
Gachagua amesema kama bosi huyo wa Usalama angemfahamisha vyema Rais Ruto kuhusu ukubwa wa maandamano hayo, maandamano yasingetokea na wala yasingefika huko.
“Habari hizi hazikupatikana kwa Rais Ruto, angejua kuwa wananchi hawakuutaka Mswada wa Fedha wa 2024 angewataka watu wake waifute. Hata hivyo, tuna shirika (NIS) ambalo limelipwa kutoa taarifa kama hizo. Ni wazi kuna kushindwa katika ujasusi,” amesema.
Pia, amesikitika kuwa kutokana na kutofanya kazi vizuri kwa NIS, maisha ya watu yamepotea na mali ya mamilioni ya fedha zimeharibiwa.
“Maofisa wakuu wameniambia kwa faragha kwamba hawakuwa na taarifa ya kijasusi kuhusu maandamano,” amesema.
Wakati huo, Gachagua ametoa wito wa kufanyika mazungumzo, ili kuepuka kujirudia kwa maandamano ya kupinga muswada wa fedha yaliyotikisa nchini humo tangu Jumanne ya Juni 18, 2024.