Mwanza. Wakati mgomo wa wafanyabiashara mkoani Mwanza ukiingia siku ya pili leo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ameitisha kikao na wafanyabiashara hao ili kujadili malalamiko yao.
Hata hivyo, viongozi wa wafanyabiashara pamoja na kupatiwa mwaliko wa kuhudhuria kikao hicho wanadaiwa kukacha, huku Mtanda akieleza kuwa milango ya ofisi yake iko wazi kwa wafanyabiashara waliofunga maduka kukutana naye, ili kutafuta mwarobaini wa suala hilo.
Akizungumza leo Jumatano Juni 26, 2024, Mtanda amesema awali hakuwa na taarifa za kuwepo mgomo huo hadi alipopigiwa simu na waandishi wa habari akiwa jijini Dar es Salaam, jambo alilodai limemfanya arejee jijini Mwanza kushughulikia suala hilo.
“Tuliwaalika wenzetu Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania ambao wao kwa kiasi kukubwa wanahusika na huo mgomo, ili tuwasikilize hoja zao tuzipime uzito wake halafu tupate suluhu, lakini mpaka sasa hawajatokea na hatuna taarifa sahihi wako wapi au kwa nini hawajafika,” amesema Mtanda.
Bila kuweka wazi msimamo wa Serikali kuhusu mgomo wa wafanyabiashara hao, Mtanda amewataka walioridhia kufungua maduka kufanya biashara yao kwa Amani, huku akidokeza wajibu wa Serikali ni kuwaimarishia ulinzi ili wasikumbane na vurugu za waliogoma.
Kiongozi huyo amesema Serikali kwa kutambua mchango wa sekta binafsi si tu kwa kuchangia kwenye pato la Taifa, pia inasaidia kuzalisha ajira kwa wananchi, huku akieleza kuwa itaendelea kushirikiana na sekta hiyo.
“Serikali itaendelea kuwa na uvumilivu kukaa nao kuwasikiliza yale mambo ya msingi yanayoweza kufanyiwa kazi yatafanyiwa, ambayo yanahusu Bunge letu ni sikivu, watasikilizwa wamepaza sauti na hayo marekebisho Bunge wameona wenyewe kwa kadri itakavyofaa.”
“Niwatake wafanyabiashara na makundi mengine kujenga utamaduni wa kukutana na kufanya mazungumzo unapokuwa na changamoto yoyote inayowasumbua. Leo tumewaita halafu hawajaja,” amesema.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati alipopigiwa simu na Mwananchi kujua sababu za kutohudhuria kikao hicho, simu yake iliita kisha kukatwa. alipopigiwa tena haikupokelewa.
Alipoulizwa kuhusu uwepo wa kero ya kodi ya huduma na ushuru wa taka, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amesema watendaji wa ofisi yake wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa Kifungu namba 6,7 na 8 cha Sheria ya Kodi namba 9 ya Mwaka 1991 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.
Kibamba amesema waliogoma ni pamoja na wafanyabiashara ambao ni wadaiwa sugu wa kodi ambao pamoja na kutoa tangazo la kuwataka kuwasilisha historia ya mauzo yao ofisini kwake hawakufanya hivyo matokeo yake alipoanza kutekeleza sheria ndipo wakaamua kugoma.
Kuhusu hasara, Kibamba amesema ofisi yake haijapata hasara kutokana na mgomo huo ulioanza jana Jumanne Juni 25, huku akidokeza kuwa makadirio ya ofisi yake jana ilikusanya Sh98 milioni, tofauti la Sh54 milioni ambazo halmashauri hiyo imeweka lengo kukusanya kila siku.
“Kwa mfano nimepeleka barua ya kuwataka wafanyabiashara kuwasilisha hesabu za mapato yao 120, lakini waliofika ofisini kwangu ni 10 tu. Sisi tutapoteza mapato ndiyo, lakini na wao (wafanyabiashara) wana mikopo benki, wanasomeshwa watoto athari ziko kote,” amesema Kibamba.
Kuhusu ushuru wa taka, Kibamba amesema hauepukiki kwa kile alichodai ofisi yake inatumia zaidi ya Sh1.7 bilioni kukusanya na kuharibu taka huku makusanyo yakiwa Sh800 milioni kwa mwaka jambo linalomlazimu kukopa angalau Sh1 bilioni kutoka vyanzo vingine vya mapato, ili kutokomeza taka jijini humo.
“Jiji la Mwanza linazalisha tani tani takribani 365 na uwezo wa kuzoa taka ni tani 233 kwa siku bampo la Buhongwa, ile mitambo ukishaiwasha inawaka Saa 24. Hivyo tunatumia takribani Sh1.7 bilioni kuzoa takataka na mchango wa wananchi, kwa hiyo lazima tuhakikishe wanalipa ili kumaliza tatizo,” amesema Kibamba.
Awali, mfanyabiashara jijini humo, Hassan Mutashobya ameiomba Serikali kuangalia upya ushuru wa taka na kodi ya huduma kwa kile alichodai utozwaji wake hauzingatii faida anayoipata mfanyabiashara.
“Kwa mfano sheria inaelekeza mfanyabiashara atozwe service levy ‘kodi ya huduma’ asilimia 0.3 kwenye faida, lakini ukifuatilia kwa kina utabaini wafanyabiashara tunatozwa zaidi ya hiyo ukienda kwenye makadirio. Tunaomba suala hili liangaliwe upya,” amesema Mutashobya.