Bukoba. Mahakama Kuu ya Tanzania, imewaamuru Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuwaachia au kuwafikisha kortini, watuhumiwa wanne wanaowashikilia mahabusu ya polisi kwa siku 15.
Amri hiyo imetolewa leo Jumatano Juni 26, 2024 na Jaji Gabriel Malata wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba wakati akitoa uamuzi wa maombi ya jinai namba 16675 ya 2024 yaliyofunguliwa mahakamani na washukiwa hao wanaoshikiliwa na Polisi.
Katika maombi hayo, watuhumiwa hao waliwashtaki Mkuu wa Polisi (OCD) wilaya ya Karagwe, Mkuu wa Upelelezi mkoa (RCO) wa Kagera, Kamanda wa Polisi (RPC) mkoa wa Kagera, IGP, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na DPP.
Watuhumiwa hao, Jasson Musolini, Johanes Johanen, Charles Dedah na Mathayo Joseph, kupitia kwa wakili wao, Jackson Mchunguzi, walifungua maombi hayo (Habeas Corpus), kuwalazimisha Polisi kuwaachia huru au kuwafikisha kortini.
Katika uamuzi wake, Jaji Malata amekubaliana na maombi yao na kuwaamuru wajibu maombi kufanya moja ya mambo manne ambayo ni ama kuwaachia huru watuhumiwa au wawafikishe kortini kwa hati ya mashtaka kwa mujibu wa sheria.
Wakishindwa kutekeleza mojawapo ya amri hiyo, basi ama wawaachie watuhumiwa hao kwa dhamana ya polisi au wazingatie matakwa yote ya kisheria kuhakikisha kuwa haki za watuhumiwa hao hazivunjwi zaidi na Polisi.
Jaji ameamuru amri hiyo itekelezwe kabla ya au ifikapo Juni 28, 2024.
Kiini cha mgogoro ni nini?
Kulingana na uamuzi huo wa Jaji akirejea kiini cha maombi hayo, amesema Aprili 2023 watuhumiwa hao walikamatwa na Polisi na kushtakiwa kortini kwa makosa ya kumiliki silaha na risasi, kinyume cha sheria na kufanya biashara ya risasi.
Hata hivyo, Juni 11, 2024 DPP amewaondolea mashtaka hayo akiegemea kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kama ilivyorejewa mwaka 2022, kwamba hana nia ya kuendelea na shauri hilo.
Baada ya kuachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya Karagwe bila masharti yoyote, mahabusu hao walikamatwa tena na Polisi mahakamani hapo na kupelekwa kituo cha Polisi cha Kayanga ambako waliwekwa mahabusu ya polisi.
Washtakiwa hao wamewekwa mahabusu katika kituo hicho tangu Juni 11, 2024 hadi Juni 17,2024 bila kufunguliwa mashtaka au kufikishwa katika mahakama yoyote ile, ndipo wakaona haki yao ya kikatiba inakiukwa na Jamhuri.
Hivyo, kupitia kwa wakili Muchunguzi, wakafungua maombi hayo ya jinai Juni 17, 2024 wakiiomba Mahakama iwaamuru wajibu maombi pamoja na mambo mengine, iwaachie huru kutoka katika kizuizi ambacho hakina uhalali kisheria.
Pia wakaiomba Mahakama iwaamuru wajibu maombi kufika mbele ya Mahakama kujieleza ni kwa nini waombaji wanaoshikiliwa kinyume cha sheria wasiachiwe huru na pia itoe amri ya kuwazuia wajibu maombi kuendelea kuwashikilia.
Wakaomba pia Mahakama itoe amri ya kuwataka wajibu maombi watimize majukumu yao kwa kuzingatia sheria na iwape nafuu itakayoona inafaa.
Majibu ya Serikali yalivyokuwa
Katika majibu yao kupitia kiapo kilichoapwa na Alice Mutungi ambaye ni wakili wa Serikali, walikuwa hawabishi kwamba mahabusu hao wako mikononi mwao hadi siku maombi hayo yakisikilizwa Juni 25, wakitimiza siku 15 wakiwa mahabusu.
Hata hivyo, katika majibu yao hayo wameeleza kuwa watuhumiwa hao walikuwa tayari wamehamishiwa wilaya ya Kasulu kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria, ingawa Jaji alisema kulikuwa hakuna ushahidi wa hicho walichokieleza Jamhuri.
Wakili Mutungi akapinga maombi hayo na kusema tayari yalikuwa yamepitwa na wakati kwa vile waombaji tayari walikuwa wamesafirishwa kwenda wilaya ya Kasulu wakisubiri kushtakiwa, hivyo suala la kushikiliwa Kayanga halipo tena.
Amesema ni kweli watuhumiwa hao walishtakiwa katika Mahakama ya Wilaya Karagwe kwa makosa ya uhujumu uchumi na kwamba wote waliachiwa baada ya DPP kuwaondolea mashtaka (Nolle Prosequi) kupitia kifungu hicho cha 91(1).
Wakili huyo ameeleza kuwa kifungu cha 29(1) cha sheria ya makosa ya kupangwa na uhujumu uchumi (EACCA) inataka mshukiwa kufikishwa kortini ndani ya saa 48 tangu kukamatwa kwake, lakini hiyo inategemea mazingira ya tuhuma zenyewe.
Akitoa uamuzi wake baaada ya kusikiliza pande mbili, Jaji amesema ni jambo lililo wazi kuwa waombaji katika shauri la sasa kuwa walikamatwa na kushtakiwa kwa uhujumu uchumi kupitia shauri la uhujumu uchumi namba 3 la 2023.
Pia Jaji amesema ni jambo lililo wazi Juni 11, 2024 DPP aliwasilisha (Nolle Prosequi) kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo, wakaachiwa bila masharti, lakini wakakamatwa tena na kuwekwa mahabusu polisi kuanzia Juni 11 hadi Juni 25.
Ameeleza kuwa hakuna ubishi kuwa tangu walipokamatwa Juni 11,2024 hadi Juni 25,2024 watuhumiwa hao walikuwa hawajashtakiwa mahakama yoyote iwe ni mkoa wa Kigoma au Kagera na wadaiwa wanaendelea kuwashikilia mahabusu.
Jaji amesema wajibu maombi wana haki ya kukamata mshukiwa yeyote wa kosa la jinai wala hilo hawalaumiwi nalo, lakini wanatakiwa watekeleze majukumu yao ikiwamo ama kuwafikisha kortini au kuwaachia kwa dhamana ya polisi.
“Hii inaifanya mahakama iamini kuwa waombaji wanashikiliwa mahabusu kinyume cha sheria kwa wajibu maombi kushindwa kutimiza wajibu hata mmoja wa kisheria zaidi tu ya kuwakamata waombaji,”ameeleza Jaji Malata.
Kwa mujibu wa Jaji Malata, vitendo vya wajibu maombi hao sita ni wazi vinakiuka takwa la lazima la kifungu cha 29(1) cha sheria ya uhujumu uchumi na kwamba kwa kile walichokieleza kortini, maombi ya watuhumiwa hao yana mashiko.
Jaji amesema kwa hali ya sasa ambapo mfumo wa haki Jinai umeboreshwa katika utendaji wa Mahakama, haitegemewi kutokea hicho kilichotokea kwa vile nchi ina miundombinu rafiki ya kutoa haki kwa wakati na haki ionekane imetendeka.
Kutokana na hilo, Jaji amewaamuru wajibu maombi hususan IGP na DPP ama kuwaachia huru kutoka kizuizi haramu ama kuwafikisha kortini, au kuwaachia kwa dhamana ya polisi na ama kuzingatia sheria ili kutoendelea kuvunja haki zao.