Dar es Salaam. Utaalamu hafifu kwa watoa huduma za afya ngazi za msingi na uhaba wa vifaatiba kubaini ugonjwa wa saratani mapema, ni sababu ya wengi kuanza tiba kwa kuchelewa.
Changamoto nyingine inatajwa ni kutokutolewa rufaa mapema inapotokea mgonjwa ana viashiria vya saratani kukua, kusambaa mwilini au kuugua mara kwa mara.
Serikali imekiri kuwapo kwa changamoto hizo, ikiainisha mikakati iliyofanyika ikiwemo usambazaji wa vifaatiba.
“Ni kweli kuna changamoto kubwa katika kuwagundua wagonjwa wa saratani mapema, hata wanapofika vituo vya afya ya msingi. Hii ni kwa zile saratani zinazohitaji vipimo vya juu kuzigundua,” anasema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Afya, Englibert Kayombo.
Anasema Serikali kupitia Wizara ya Afya na Taasisi ya Saratani Ocean Road inaendelea kupunguza tatizo hilo kwa kutoa huduma ya kupima saratani mapema katika vituo 800 nchini na kusambaza mashine za ultrasound, x-ray na CT-scan katika hospitali zote za mkoa.
“Kwa sasa takwimu za Ocean Road zimeanza kuonyesha matunda. Mfano, kiwango cha wagonjwa wanaofika hatua za juu (3 na 4) miaka 10 iliyopita kilikuwa asilimia 70-80, lakini kwa sasa ni asilimia 40-50, ikimaanisha wanaowahi wakiwa hatua za awali wanakaribia nusu ya wagonjwa wote,” anasema.
Kayombo anataja juhudi nyingine zilizofanyika ni kusambaza mashine kubwa za kisasa za MRI kwa hospitali zote za rufaa za kanda nchini.
Anasema kumekuwa na kampeni zinazoambatana na kupima saratani, elimu kupitia vyombo vya habari na kuendelea kufanya tafiti katika vyanzo, tiba na kinga za ugonjwa huo nchini.
“Pia kutoa chanjo maalumu kwa watoto ya virusi vinavyohatarisha saratani kama HPV kwa shingo ya kizazi na HBV kwa saratani za ini,” anasema Kayombo.
Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Saratani Tanzania (TOS), Dk Jerry Ndumbaro anasema ni muhimu kuwawezesha madaktari wa ngazi ya chini kuanzia zahanati, vituo vya afya na wilaya katika kutambua mapema dalili za magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani.
Anasema TOS kwa kushirikiana na TNCDA ambao ni mwamvuli wa vyama vya magonjwa yasiyoambukiza na Wizara ya Afya walifanya mafunzo nchi nzima miaka mitatu iliyopita.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wanatakiwa kuongeza nguvu katika hili ili magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo saratani, yagunduliwe mapema,” anasema.
Dk Ndumbaro ameshauri kuongeza upatikanaji wa vifaatiba vya patholojia (vinavyotumika kubaini saratani) na dawa hasa kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani.
Anaitaka Serikali kuhimiza rufaa za mapema kutoka ngazi moja ya afya kwenda nyingine ili wagonjwa wasichelewe kupata tiba, maana matibabu ya saratani kwa sasa yanapatikana katika hospitali zote ngazi ya kanda na hospitali za rufaa.
“Kwenye saratani ya kizazi kumeonekana wagonjwa wanaanza wengi kuja hasa Taasisi ya Saratani Ocean Road wakiwa hatua za awali kutokana na vituo vya kupima saratani hii kusambaa nchi nzima, kuanzia ngazi ya hospitali za wilaya,” anasema Dk Ndumbaro.
Mkuu wa Idara ya Saratani Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Nestory Masalu anasema changamoto kubwa wananchi wengi hawajui dalili za saratani.
Anasema kutokuwapo vifaatiba vya kugundua saratani ngazi ya chini na uchumi duni kwa baadhi ya familia kumudu vipimo vya ugonjwa huo husababisha baadhi kuishia kutumia tiba asilia.
“Wakiambiwa uchunguzi hawapimi, wengi wanaenda kwa waganga wa jadi, vituo vinavyoweza kupima saratani ni vichache,” anasema.
Mbali ya hayo, anasema woga ni sababu nyingine akieleza: “Elimu zaidi inahitajika, tuelimishe jamii ijue kuna uchunguzi wa awali. Bima zifikirie namna ya kuweka kinga kuwa sehemu ya matibabu kwa maana hakuna sehemu ambako bima itagharimia uchunguzi wa awali wa saratani.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Dk Gilead Massenga anasema kuna changamoto ya wagonjwa kufika vituoni kutibiwa kitu kingine ilhali ana dalili za wazi za saratani, hivyo elimu zaidi kwa wataalamu ngazi za chini ni muhimu ili wawape rufaa mapema.
“Vituo vya msingi wakipata elimu itakuwa rahisi kuwafikisha wagonjwa katika hatua za awali,” anasema Dk Massenga.
Mwanzoni mwa Februari 2021, Rukia Muktwaf (sasa marehemu) aliyeishi Mbagala alianza kuugua, licha ya kufika zahanati, kituo cha afya na baadaye Hospitali ya Mbagala Zakheim wataalamu wa afya hawakugundua nini kinamsumbua.
Machi 2023, Rukia (45) alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Temeke alikochukuliwa sampuli kutoka kwenye ziwa lake iliyopelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi.
Baada ya miezi kadhaa ndipo akapewa rufaa ya kwenda Ocean Road Oktoba, 2023.
Mwanaye Amina Sephu, akizungumza na Mwananchi anasema mpaka mama yake alipofariki dunia Novemba 4, 2023 hakuondolewa titi lililokuwa limeathiriwa na saratani kwa kiwango kikubwa, hivyo ugonjwa ulisambaa hadi kwenye mifupa.
“Mama alienda hospitali mapema akiwa anatembea na nguvu zake tangu alipoona mabadiliko na homa za mara kwa mara. Miaka miwili alikuwa akitibiwa hospitali za chini na hata alivyowaambia anaona mabadiliko kwenye ziwa la kushoto, iliwachukua muda kumpa rufaa kwenda Temeke,” anasema.
Amina anasema kwa kipindi cha miezi 16 tangu kuanza kuugua, nyonga ya mama yake iliachia na baadaye bega la kushoto, wataalamu wakawaeleza saratani ilishasambaa kwenye mifupa, na tangu hapo alikuwa wa kubebwa hakuweza kutembea tena.
Kwa upande wake, Shukran Ngatale (41) anayeendelea kutibiwa saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, anasema alihudhuria zahanati, vituo vya afya na hata hospitali kwa zaidi ya miezi 10, hata hivyo wataalamu wa afya hawakubaini tatizo mapema.
Changamoto hii, iliyompata Shukran inaungwa mkono na wanawake watano wanaoendelea kutibiwa saratani ya shingo ya kizazi katika taasisi hiyo kwa sasa.
Shukran anasena alihangaika kutibu tatizo la kutokwa damu mfululizo kwa miezi 10 tangu Machi, 2023.
“Tatizo lilidumu muda mrefu bila kujua naumwa nini, nimeenda hospitali nyingi halikugundulika, baadaye nikaenda Ikonda, wilayani Makete mkoani Njombe. Pale walinichukua kipimo cha sampuli ya nyama kwenye kizazi, baada ya siku 14 wakabaini nina saratani,” anasimulia.
Mei 2, 2024 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema takwimu za ufuatiliaji kupitia ripoti ya Globocan zinaonyesha takribani wagonjwa wapya wa saratani 40,000 hugunduliwa kila mwaka na watu 27,000 wenye ugonjwa huo hufariki dunia nchini.
Alisema sehemu kubwa ya wagonjwa wa saratani nchini wamebainika kuwa ni wanawake wenye saratani ya mlango wa kizazi wanaochangia asilimia 25, ikifuatiwa na saratani ya matiti kwa asilimia 10.
Kwa pamoja saratani hizo zinachangia zaidi ya asilimia 33 ya wagonjwa wote, huku zikichangia nusu ya vifo vyote vya saratani.
Hata hivyo, alisema vifo vitokanavyo na saratani vitaongezeka ifikapo mwaka 2030 kama hatua za kushughulikia ukubwa wa tatizo hilo hazitachukuliwa nchini. Inakadiriwa kufikia vifo milioni moja mwaka 2030
Kutokana na wagonjwa kufika hospitali katika hatua za juu za ugonjwa, wataalamu wa afya wanahimiza elimu kwa umma itolewe licha ya kuelimisha wataalamu katika ngazi za msingi.
“Suala hili lina pande mbili, uelewa kwa jamii na watoa huduma. Jamii tumekuwa tukisema ni vizuri wananchi wawe na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya hata kama hauumwi angalau kila mwaka mara moja,” anasema Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deus Ndilanha.
Anasema hilo litaibua watu wengi wenye changamoto za magonjwa na kuwaingiza katika hatua za matibabu mapema.
“Wataalamu wanapaswa kukumbushwa wakiona kitu si cha kawaida kwa mgonjwa hasa uvimbe wafikirie yaweza kuwa saratani, wampe rufaa kwenda hospitali kubwa kuchunguzwa mapema,” anashauri.
“Ukiona mwanamke anatokwa damu mfululizo kama si njia ya uzazi wa mpango aliyotumia, wafikirie kumpa rufaa kuchunguzwa saratani ya kizazi. Tabibu amepata mgonjwa ambaye anaona ugonjwa upo juu kuliko yeye anavyoweza kumtambua ampe rufaa,” anasisitiza.
Licha ya wataalamu bingwa wa magonjwa ya saratani kutoa mafunzo kwa huduma mkoba, ugunduzi wa mapema kwa wagonjwa umeendelea kuwa mgumu.
Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa Hospitali ya Ocean Road, Islam Mposso anasema wataalamu bingwa wa magonjwa ya saratani wameendelea kuwapa elimu wataalamu ngazi za chini.
“Tunavyoenda kutoa huduma mkoba ngazi za chini, huwa tunatoa elimu kwa watoa huduma kwa kushirikiana nao kwa asilimia 100 kupima saratani ya mlango wa kizazi na nyinginezo,” anasema.
Anasema huwapokea wagonjwa waliochelewa wakiwa hatua ya tatu au ya nne ya ugonjwa hivyo matibabu kuwa ya gharama zaidi.