Wakulima wa pamba walalamikia mizani kuchakachuliwa

Mwanza. Wakulima wa zao la Pamba mkoani hapa wamelalamikia baadhi ya wanunuzi kuchakachua mizani inayotumika kununulia zao hilo, hali inayowasababishia kupata hasara.

Wakizungumza leo Jumatano Juni 26, 2024 na Mwananchi, wakulima hao wamesema kitendo hicho kinawafanya baadhi yao kukata tamaa na kushindwa kuendelea na kilimo hicho.

“Mizani inayokuja kupima pamba tunaomba wapimaji wasiwe wanaichezea na kuchakachua, unaleta pamba nyingi, lakini unajikuta umetoa kilo chache sana tofauti na matarajio, sasa inatakiwa wawe wanapima vizuri wasiwe wanachakachua mizani,” amesema Mussa Fulument, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Kadashi.

Akiunga mkono hoja hiyo, Asteria Cosmas, mkazi wa Kijiji cha Bugandando wilayani Kwimba ameiomba Serikali kupitia Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, ili kuwachukulia sheria watakaobainika kuchakachua mizani hiyo. 

“Ukaguzi ukiwa unafanyika mara kwa mara wakulima wa pamba tutakuwa tunafaidika na zao letu, kwa sababu kama mzani utakuwa vizuri na mimi mkulima nitapata manufaa makubwa na kunipa tija ya kuendelea kulima,” amesema Asteria.

Mawakala washtukiza ukaguzi wa mizani

Kutokana na malalamiko hayo, Wakala wa Vipimo mkoani Mwanza umefanya ukaguzi wa kushitukiza katika vituo vya kununulia zao hilo vinavyoratibiwa na Vyama vya Ushirika (Amcos) kwa lengo la kuwachukulia sheria wale wote watakao bainika.

Akizungumza na Mwananchi wakati wa ukaguzi huo wakiwa wilayani Kwimba, Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kagera, Johnstone Japhet amesema oparesheni hiyo imeanza tangu Juni 24, mwaka huu baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Kilichotusukuma kufanya oparesheni hii ni baada ya tafiti kufanyika na kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba kuna mizani inatumika lakini imechezewa, kwa hiyo Wakala wa Vipimo akawa ameunda kikosi kazi kuja kufuatilia hayo malalamiko ya baadhi ya wakulima wa pamba na sasa tunayafanyia kazi, ili kuona kama yana ukweli,” amesema.

Amesema ukaguzi huo waliuanza Wilaya ya Magu na leo walikuwa Wilaya ya Kwimba, kesho wataendelea na wataufanya kwa siku nne mfululizo.

“Mpaka mpaka leo tumekagua Amcos 14 kati ya hizo Amcos, mbili tumekuta mizani yao ina changamoto na tayari hatua za kisheria zimechukuliwa, mmoja amelipa faini tayari na mwingine taratibu za kisheria zinaendelea kuchukuliwa,” amesema Japhet.

Hata hivyo, ametoa angalizo kwa wafanyabiashara na viongozi wa vyama vya ushirika kukaguliwa mizani yao, kwani kushindwa kufanya hivyo adhabu yake ni kuanzia Sh100,000 mpaka Sh20 milioni.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa Vipimo, sura namba 340 mtu asipokaguliwa mzani wake ni kosa kisheria na sheria imeelekeza anaweza kutozwa faini ya Sh100,000 mpaka Sh20 milioni kwa hiyo kama mzani wako haujakaguliwa upeleke ofisi ya wakala wa vipimo iliyokaribu yako ukaguliwe,” amesema Japhet.

Amcos wazungumzia malalamiko

Viongozi wa vyama vya ushirika katika maeneo ya wakulima wa pamba walipoulizwa kuhusiana na hilo, wamedai wakulima ndio chanzo, kwani huchanganya maji na mchanga kwenye pamba ili kilo kuongezeka.

“Ni kweli hilo lipo, ila siwezi nikasemea watu wengine, lakini na wao wakulima wanachangia wakati mwingine wanapokuwa wakileta pamba yenye maji na mchanga, hiyo inafanya iwe vita sasa kati ya wanaopima na wanaoleta kwa sababu ikiletwa pamba ambayo ina mchanga ndani yake ndio inasababisha waharibu mzani ndani kitendo ambacho si halali,” amesema Elisha James, Katibu wa Amcos katika Kijiji cha Kadashi Kata ya Maligisu Wilaya ya Kwimba

Akiunga mkono hoja hiyo, Katibu wa Amcos eneo la Nyahanga wilayani Kwimba, Lucas Sayayi amesema ukaguzi huo ni muhimu kwao na kwa wakulima, kwani huongeza motisha kwa wakulima kulima zaidi, huku wakiamini watapata faida kubwa.

“Niwapongeze Wakala wa Vipimo kwa kututembelea katika maeneo yetu na kukagua mizani, huku wakulima wakiona kwa sababu hii inasaidia kuongeza motisha kwa wakulima kulima zaidi zao la pamba kwa sababu wanapata kile walichovuna maana kipimo kikiwa sio halali wakulima wanakata tamaa kwa sababu anapata tofauti na jinsi kilo zilivyo,” amesema Sayayi.

Related Posts