Moto Ligi U-17 kuwaka Leaders, Dar Gymkhana

Viwanja mduara vya Leaders na Dar es Salaam Gymkhana ndivyo vitaamua timu ipi ni bora katika Ligi ya Vijana chini ya umri wa miaka 17, jijini Dar esa Salaam wikiendi hii.

Kwa mujibu wa msemaji mkuu wa chama cha kriketi nchini (TCA), Ateef Salim, ligi hii ina upinzani mkali kwani inajumuisha vijana wenye damu changa na nia ya kuwa wachezaji nyota kwa taifa hili siku zijazo.

Mechi ya kwanza itazikutanisha Chanika Boys na Indian School katika viwanja vya Leaders Club Jumamosi hii, huku Ilala Boys  na Future Force Academy zitakipiga Uwanja wa Gymkhana na yote ikiwa ni ya mizunguko 10 (10 overs).

Ligi ya Caravans T20 pia itaendelea wikiendi hii baada ya mechi kali kadhaa mwishoni mwa juma lililopita. 

Mmoja wa wababe wa ligi hii ya mizunguko 20 (T20) ni Alliance  Caravans waliotoka kifua mbele Jumapili baada kuwanyanyasa Econo Lodge Lions kwa mikimbio 111, kwenye viwanja vya Leaders.

Alliance Caravans ndio waliotengeneza mikimbio mingi (194), huku wakipoteza wiketi 6 na alama hizo zilionekana ngumu kwa Econo Lodge kuzifikia baada ya wote kutolewa wakiwa na mikimbio 83 tu.

Katika mchezo huo, Prakash Nair wa Alliance aliyetengeneza mikimbio 103 (century) peke yake, huku Jerry Mathew akiongeza mikimbio 33.

Annadil Burhan pia walikuwa na siku nzuri dhidi ya Estim B katika mchezo wa mizunguko 30 (30 overs) uliofanyika jijini mwishoni mwa wiki.

Burhan walioanza kwa kulinda baada ya wapinzani wao kupata kura ya kuanza, walishinda Estim B kwa wiketi saba baada ya kuifikia mikimbio 139 ya Estim B ambao walimaliza kwa kuangusha wiketi 8. Burhan walishinda baada kutengeneza mikimbio 143 huku wakiangusha wiketi tatu tu.

Vilevile kulikuwepo na mechi ya Ligiya Daraja la Tatu katika mfumo wa ova 20.

Patel B waling’ara dhidi ya DJ Fighters kwa ushindi wa wiketi moja.

DJ Fighters walioshinda kura ya kuanza, walifanikiwa kupata mikimbio 74 huku wakiangusha wiketi zote 10, huku Patel B walifikia alama hiyo kwa kupata mikimbio 75 na kupoteza wiketi 9.

Related Posts