WAKALI 38 wanatarajiwa kuchuana katika mashindano maalumu ya kumuenzi Lina Nkya ya Lina PG Tour, kwenye viwanja vya Gymkhana, jijini Arusha, Julai 11 hadi 14, mwaka huu.
Mashindano haya yanayoingia raundi ya tatu kati ya tano, yanamuenzi nyota huyo ambaye enzi za uhai wake alifanya kazi kubwa ya kuilea gofu ya wanawake kwa mafanikio hadi kuwafanya kinadada wa Kitanzania kung’ara katika mashindano mbalimbali Ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika na mashindano ya dunia yaliyofanyika Argentina muongo mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa mashindano haya, Yasmin Chali kutoka familia ya Lina Nkya, hadi jana, wachezaji 38 wameshajisajili kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo.
Wacheza gofu ya kulipwa Nuru Mollel aliyeshinda raundi ya kwanza katika viwanja vya TPC Moshi na Hassan Kadio aliyeutwaa ubingwa wa raundi ya pili mjini Morogoro, ni baadhi ya waliosajiliwa kucheza katika raundi hii ya tatu.
Pia Ally Isanzu aliyeshinda raundi zote mbili za mashindano hayo katika viwanja vya TPC, mwezi Machi na viwanja vya Gymkhana Morogoro mwezi Aprili mwaka huu, ndiye anayeongoza orodha ya wachezaji 19 wa ridhaa watakaowania taji na zawadi katika viwanja vya Gymkhana Arusha, kwa mujibu wa Chali.
Aliongeza, wachezaji hao 38 walijisajili hadi Mei 31 mwaka huu, siku ya mwisho ya kujisajili kwa ajili ya mashindano haya na jumla ya mashimo 72 yatachezwa katika siku hizo nne, ikiwa na maana kutakuwa na mbio za mashimo 18 kila siku.
Akifafanua, Chali alisema wachezaji wa ridhaa wanaokubalika kushiriki mashindano ya mwaka huu ni wale wenye kiwango pungufu cha tano (5 handicap).
“Kila kitu kinakwenda vyema katika maandalizi yetu na viwanja vya gofu vya Arusha viko katika ubora unaotakiwa kwa ajili ya mashindano haya,” alisisitiza Chali na kuongeza pia kutakuwa na mashindano kwa ajili ya wachezaji wa kawaida (Subsidiary event).