Mbeya,
27.6.2024
Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inatarajia kuendesha programu ya mafunzo ya ujasiriamali kwa wajasiriamali 50 waliopo katika Halmashauri saba zinazotekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai Tanzania (SLR).
Mafunzo hayo ya mfumo wa kidijitali yatahusisha shughuli za wajasiriamali zinazohamasisha urejeshaji wa mifumo ya ekolojia asilia na hifadhi ya mazingira zinazolenga kuwaongeza kipato kupitia fursa za biashara.
Akizungumza katika kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa shughuli za mradi kwa mwaka 2024 Juni 26, 2024, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda amesema mafunzo pia yatasimamiwa kwa karibu na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Shirika la Anza Tanzania na Shirika la Bridge for Billions.
Dkt. Mapunda amesema mafunzo hayo yamekusudia kuwajengea uwezo wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi kuweza kuibua fursa za biashara na ujasiriamali, ushauri wa kitaalamu na ufadhili wa miradi mbalimbali itakayoibuliwa na vikundi vya kijamii.
Amefafanua kuwa walengwa wa programu hiyo ni wajasiriamali wanaofanya shughuli endelevu za uhifadhi wa mazingira katika Bonde la Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa ikihusisha Halmashauri za Wilaya ya Iringa, Mbarali, Mbeya, Mpwimbwe, Tanganyika, Wanging’ombe na Sumbawanga.
“Programu hii ni fursa nyingine iliyopo ndani ya mradi unaotekelezwa katika Mataifa 10 Duniani mradi…Timu ya wataalamu wezeshi imeanza ziara katika Halmashauri husika, nawasihi maafisa maendeleo ya jamii kutoa elimu kwa vikundi mbalimbali ili viweze kuchangamkia fursa hii” amesema Dkt. Mapunda.
Aidha ameongeza kuwa mafunzo hayo yatagusa shughuli wezeshi za uhifadhi wa mazingira ikiwemo uchakataji wa mazao ya misitu, ulinzi wa vyanzo vya maji, utalii wa mazingira, vitalu vya miti, ufugaji, kilimo, watengenzaji wa majiko na nishati safi pamoja na mkaa mbadala.
Kwa mujibu wa Dkt. Mapunda amesema kupitia mafunzo hayo, wananchi waliopo katika Halmashauri husika wataweza kuanzisha miradi ya endelevu ya kibiashara inayostahimili mazingira na kuchochea urejeshaji endelevu wa mifumo ikolojia ndani ya maeneo ya mradi.
Kwa upande wake, Mshauri wa Kiufundi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Bw. Doyi Mazenzele akiwasilisha mada katika kikao hicho, amesema programu hiyo imelenga kuwawezesha wananchi waliopo katika maeneo ya mradi kuweza kuibua mawazo ya biashara na miradi kwa ajili ya kujiongezea kipato katika ngazi ya kaya na familia.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanaendeshwa katika kipindi cha muda wa miezi sita kuanzia Julai 2024 hadi Februari 2025 na kuwataka wananchi waliopo katika Mikoa na Halmashauri zinazotekeleza mradi kujitokeza ili kuchangamkia fursa hiyo.
“Mafunzo haya yakikamilika mnufaika anatarajia kupatiwa kiasi cha Dola 5000 kwa ajili ya kuanza biashara kupitia miradi iliyoanishwa katika mafunzo yatakatolewa kati ya wiki 6-8 na wanufaika watapatiwa kompyuta mpakato kwa ajili mafunzo” amesema Mazenzele.
Aidha Mazenzele amesema katika kurasimisha mafunzo hayo, Ofisi yake tayari imefanya mawasiliano na Taasisi za Serikali zinazosimamia mafunzo ya wajisiriamali ikiwemo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ili kuhakikisha mafunzo hayo yanatambulika katika ngazi mbalimbali.
Mradi wa SLR unaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 25.8 unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitano unaotarajia kukamilika mwaka 2025, ulianza mwaka 2021 ukihusisha jumla ya Mikoa mitano, Halmashauri saba, Kata 18 na vijiji 54.
Halmashauri za Wilaya zinazonufaika na mradi huo ni Iringa Vijijini, Wanging’ombe, Mbeya Mbarali, Sumbawanga, na Mpimbwe.