Arusha. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amewasili mkoani Arusha kwa lengo la kuongeza nguvu kwenye kambi ya madaktari bingwa na wabobezi inayoendelea jijini Arusha.
Profesa Janabi amewasili usiku wa kuamkia leo ambapo leo Alhamisi Juni 27, 2024 ataungana na timu ya wataalamu wanaoendelea kutoa huduma na jukumu lake kubwa litakuwa kutoa elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kutibu wagonjwa binafsi.
Akizungumza baada ya kuwasili mkoani hapa, Profesa Janabi amesema timu kubwa ya madaktari kutoka hospitali ya Muhimbili iko hapo tangu siku ya kwanza na timu hiyo kwa ujumla itaendelea kuangalia magonjwa ya kuambukiza.
“Kesho nitakuwepo kwenye kambi kubwa, mchango wangu utakuwa kutoa elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza yote; kwa umuhimu wake, saratani, moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu, figo, tunachokiona nini wananchi wanaweza kuepuka.
“Kwa sababu haya magonjwa yanaepukika, ni muhimu kuchukua kinga, sehemu ya muda nitatumia kuona wagonjwa binafsi, kupata ripoti kutoka kwa wenzangu waliotangulia huku na kuangalia wagonjwa wangapi watatibiwa hapa, KCMC na baadhi watakaokuja Muhimbili,” ameongeza.
Mkurugenzi huyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo ambayo inatolewa bure.
Wakati huohuo, Taasisi ya Utoaji Huduma za Afya Aga Khan Tanzania imetoa chumba maalumu cha kuhifadhia dawa baridi chenye thamani ya Sh56 milioni kwa ajili ya kuhifadhi dawa na chanjo kwenye kambi hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi chumba hicho, Meneja Miradi wa Aga Khan, Theresia Mhere amesema chumba hicho cha dawa kina uwezo wa kubeba chanjo zaidi ya milioni moja na baada ya kukamilika kwa kambi hiyo kitapelekwa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kuhifadhi dawa.
“Aga Khan iliona ni vema kuunga juhudi za Serikali mkono na kuhifadhi chumba hiki chenye uwezo wa kubeba chanjo zaidi ya milioni moja kwa wakati mmoja na tuko tayari kushirikiana wakati wowote,” amesema.
“Tunamshukuru Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye tumekuwa tukifanya naye kazi kwa karibu na tulipomueleza kuhusu hili akawa ameshauri kitapelekwa Halmashauri ya Karatu kwa ajili ya kuendelea kuhifadhi chanjo katika halmashauri ile,” ameongeza.