MWENYEKITI WA CCM TANGA ACHUKIZWA NA UBABE WA WATENDAJI

Raisa Said,Handeni

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajab Abdulrahman ameendelea kusisitiza viongozi kutekeleza agizo la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alilolitoa hivi karibuni kuwataka viongozi na watendaji wote kuacha kutumia mabavu kwa wananchi wanaowaongoza.

Kali hiyo ameitoa wilayani Handeni katika ziara yake alipofika kukagua ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Kibaya kata ya Misima ambapo wananchi wa kijiji hicho wameeleza kutokushirikishwa kwenye miradi huku wakidai kukamatwa na kupelekwa Polisi.

Aidha wananchi wa kijiji hicho wamewalalamikia viongozi wao kutowashirikisha kwenye maamuzi pamoja na miradi inayotekelezwa hususani katika ujenzi wa zahanati hiyo ambayo inajengwa kwa nguvu za wananchi na michango ya wadau mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga ambaye hadi sasa ameshawachangia zaidi ya sh million tano na nusu .

Rajabu amewataka viongozi wakae pamoja na wananchi wa kijiji hicho cha Kibaya ili kuondoa tofauti zilizopo ambapo kati ya vitongoji vinne vilivyopo ni wananchi wa vitongoji viwili pekee ndio wanaoshiriki katika ujenzi wa zahanati hiyo.

“Kijiji hiki kina vitongoji vinne zahanati hii ni ya vitongoji vyote haiwezekani wananchi wa vitongoji fulani hawashiriki wanashughulika wengine lazima wananchi wa vitongoji vyote nao washiriki katika mradi huu kutoa nguvu zao,viongozi niwaelekeze twendeni tukakae nao kwanini hawashiriki kisha baada ya hapo tuondoe tofauti hizo,kuhakikisha kwamba mgogoro huu unamalizika lakini mradi huu lazima uendelee kama tulivyokusudiwa ili kuwapunguzia na kuwaondolea wananchi adha hizi za kukosa huduma ya afya karibu”

” Viongozi wenye kutumia ubabe Mheshimiwa Rais hataki kuwaona kabisa viongozi hao , ubabe wa nini ? wewe unawaongoza watu wenye akili zao timamu na maarifa kama wanakosea wajibu wako kama kiongozi unapoona wananchi wanalalamika ujue kuna tatizo sio bure “

Awali akizungumza mmoja wa wananchi wa kijiji hicho cha Kibaya Hamza Mzimu amesema kuwa eneo hilo hakuna huduma za afya karibu,hivyo inawabidi kutembea kilomita saba,sawa na kilomita 14 kwenda na kurudi kata ya jirani kufuata huduma ya afya.

Amesema changamoto hiyo imekuwa ikiwaathiri zaidi hasa wanawake ambao wanahitaji huduma za kliniki pamoja na wajawazito,hivyo wanamshukuru Mwenyekiti Rajabu kwa kuamua kujitoa kuwasaidia katika ujenzi huo ambao alisema utakuwa mkombozi kwa wananchi wote wa kijiji hicho

“Hapa inatubidi kutembea umbali wa kilometa saba kwenda kata ya jirani kufuata huduma za afya,wanawake ndio wanateseka zaidi kwa kutembea umbali mrefu,hivyo ujenzi wa zahanati hii ni muhimu sana kwetu “,Alieleza Mwananchi huyo.

Mkuu wa wilaya ya Handeni Albert Msando amekiri kuwepo mgogoro huo ulianza Februari mwaka huu,ambapo ofisi yake kwa kushiriki na chama waliutatua na ndio sababu ujenzi umeanza.


Related Posts