Geita Gold inaendelea kupoteza wachezaji wake baada ya kushuka daraja, ambapo safari hii ni mshambuliaji wake, Ramadhan Kapera ambaye ameachana na timu hiyo kutokana na sharti la mkataba aliousaini dirisha dogo.
Kapera aliyesajiliwa dirisha dogo na timu hiyo akitokea Mbeya Kwanza akiwa na mabao tisa Championship, na kusaini mkataba wa mwaka mmoja ambao ulikuwa na kipengele cha kuvunjika endapo Geita ingeshuka daraja kutoka Ligi Kuu.
Hatua ya Geitakushuka daraja msimu uliopita kinamfanya mshambuliaji huyo ambaye hakupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na ushindani wa namba klabuni hapo, kuwa huru na kuanza kuzivutia timu za Ligi Kuu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kapera alithibitisha kumalizana na Geita na kwa sasa yuko huru, huku akianza mazungumzo na baadhi ya timu za Ligi Kuu ambazo zinavutiwa na huduma yake na KenGold, Tanzania Prisons zinatajwa kumnyatia nyota huyo.
“Mimi na Geita tumeshamalizana nilisaini mwaka mmoja na kipengele cha timu ikishuka tunaachana, kwa hiyo hawanidai labda mimi ndiyo nawadai,” alisema Kapera na kuongeza;
“Kwa sasa natengeneza mazingira nipate timu ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao, kwa hiyo kuna baadhi ya timu tayari tumeshaanza mazungumzo na mambo yakikamilika mtajua.”
Ofisa Habari wa Geita Gold, Samwel Dida, alisema uongozi wa timu hiyo unajiandaa kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi chao ambacho kitakuwa ghali zaidi kwenye Ligi ya Championship kikiwa na hadhi ya Ligi Kuu na kwa sasa wanasubiria maamuzi ya mwisho ya kupitisha bajeti.