Dodoma. Bunge la Tanzania limeelezwa mikakati inayofanywa na Serikali kwa ajili ya kupambana na vitendo vya ukatili ikiwemo kutoa huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kwa jamii na kutoa hifadhi ya dharula kwa manusura wa vitendo vya ukatili.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Wingwi (CCM) Omaari Issa Kombo, leo Alhamisi, Juni 27, 2024.
Mbunge huyo amehoji Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwemo mauaji yanayotokea kwenye jamii kwa sababu za wivu wa kimapenzi.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi amesema Serikali inayo mikakati mbalimbali inayolenga kutokomeza ukatili dhidi ya watoto hapa nchini.
“Mikakati hiyo pamoja na kuboresha vituo vya huduma kwa wateja ili kuwawezesha wananchi kupata elimu na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa wakati,” amesema.
Amesema mingine ni kutoa huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kwa jamii na kutoa hifadhi ya dharula kwa manusura wa vitendo vya ukatili.
Mwanaidi amesema mikakati mingine ni kuratibu madawati ya jinsia katika maeneo ya umma na kuwezesha wananchi kiuchumi, kuimarisha uendeshaji, usimamizi na uratibu wa mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa.
“Mikakati hiyo imebainishwa katika Mpango Kazi wa Taifa wa Pili wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na Sera ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya Mwaka 2023 kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwemo mauaji yanayotokea kwenye jamii kwa sababu za wivu wa kimapenzi,” amesema Mwanaidi.
Katika swali la nyongeza, Kombo amesema mikakati ya Serikali ni mizuri ya kupambana na changamoto hiyo lakini hajaona ushirikishwaji wa jamii dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.
“Je Serikali haioni haja ya kushirikisha moja kwa moja jamii kupambana na vitendo hivi kama wanavyofanya Jeshi la Polisi katika dhana ya ulinzi shirikishi,” amehoji.
Pia amesema vitendo hivyo vingi vinatokea katika jamii ambapo Watanzania wanapoteza maisha na kuhoji Serikali haioni haja ya kushirikiana na viongozi wa dini katika kuwapa elimu wananchi.
“Kwa sababu vitendo hivi vinasababishwa na mmomonyoko wa maadili vile vile na wananchi kupoteza hofu ya Mungu na wanaojenga hofu ya Mungu ni viongozi wetu wa dini. Sasa Serikali haioni haja ya kushirikisha viongozi wa dini,”amesema.
Akijibu maswali hayo, Mwanaidi amesema Serikali imekuwa ikishirikiana na jamii katika kutekeleza afua za ulinzi na ndio maana kamati zao zinaanzia katika vijiji hadi katika ngazi ya Taifa.
Pia, amesema Serikali inashirikiana na viongozi wa dini katika kutekeleza mpoango wa pili wa Mtakuwa na kuwa viongozi hao wako katika kamati za ulinzi na usalama.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rose Tweve amesema kwa kuwa vitendo vya ukatili na unyanayasaji wa kijinsia vimekuwa vikijitokeza kila mwaka na kuhoji kama Serikali iko tayari kupitia vifungu vya sheria ambavyo vimekuwa vikikinzana na kuchochea changamoto hiyo.
“Kwa sababu sheria yetu inatambua kijana aliye na umri wa miaka 18 anaweza kuoa na kuolewa na anaweza kupiga kura kwa sababu anatambua mazuri na mabaya. Lakini ukija katika adhabu kijana mwenye umri huo na chini miaka 18 ambaye amelawiti ama kubaka adhabu yake ni siku 30 na kuchapwa viboko,” amesema.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi amesema Serikali kwa kushirikiana Tume ya Kurekebisha Sheria iko katika hatua ya kuendelea kurekebisha sheria za adhabu na watakapokamilisha watapeleka bungeni kwa ajili ya kurekebishwa.
“Ili kuhakikisha adhabu zinazotolewa ni stahiki kwa mtuhumiwa ambaye vitendo hivyo vya ukatili,” amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mariam Azzan Mwinyi amesema ni hivi karibuni mtoto mwenye ulemavu katika Wilaya ya Sengerema amenusurika na kifo na kuhoji Serikali inatoa tamko gani kuhusu jambo hilo ambalo linaanza kutoa mizizi mikubwa nchini.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Ndalienanga amesema Serikali imeshatoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa yote na wakuu wa wilaya kuhakikisha kuwa wanaimarisha ulinzi kwa watu wenye ualibino.
“Lakini tuseme tunaendelea kuwapa elimu watanzania waendelea kuwapenda na kuwadhamini watu wenye ualbino ili wasiwadhuru na sisi tunaendelea kufuatilia kwa karibu jambo hili. Na tunawataka walezi waendelee kuwa karibu na watoto hawa,” amesema.