NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni amewaonya Viongozi wa Serikali za Vijiji kuacha tabia ya kupokea wafugaji wageni kinyemela hasa kipindi cha kiangazi ambao ndiyo chanzo cha kutokea migogoro ya Wakulima na Wafugaji.
Ametoa maelekezo hayo Kata ya Saweni akiwa kwenye muendelezo wa ziara zake za kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wakazi wa Same kupitia mikutano ya hadhara ambapo amesema Viongozi wa Serikali za Vijiji wanapaswa kutimiza jukumu lao la msingi la kusimamia usalama na amani kwenye maeneo yao.
“Sasahivi tunaelekea kwenye kipindi cha ukame sihitaji migogoro ya Wakulima na Wafugaji kwa sababu kwenye wilaya yetu maeneo ya Wakulima na Wafugaji yanafahamika kisheria naomba kila mmoja akae kwenye eneo lake kuanzia sasa tusitiane hasara” alisema Kasilda.
Aidha amesisitiza Viongozi wa Serikali za Vijiji kuhakikisha kipindi mifugo inapoingia kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao ni vyema wakasimamia kikamirifu sheria zilizoweka kutatua migogogoro hiyo ili kuepusha pande hizo mbili zenye mgogoro kujichukulia sheria mkononi na kuhatarisha usalama.
Pia amewataka wananchi pindi wanapokamata mifugo ikiwa imefanya uharibifu kwenye mashamba yao ni vyema wakatoa taarifa haraka kwa Viongozi wa Serikali za Vijiji na Jeshi la Polisi waweze kufika eneo la tukio kutoa msaada pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa vinavyoweza kufanywa na baadhi ya viongozi wasio waadilifu vitakavyopelekea mkulima kukosa haki yake.
Awali wakitoa kero na malalamiko yao kwa Mkuu huyo wa Wilaya baadhi ya wakazi wa Kata hiyo wamesema kumekuwepo na matukio ya Wafugaji kuvamia mashamba na kulisha mifugo kwenye mazao ya wakulima hali inayopelekea kuwepo kwa migogoro isiyo ya lazima.
Kwaupande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Jimson Mhagama akijibu malalamiko hayo amesema iwapo mifugo itakamatwa kwenye shamba la mkulima anaitwa bwana shamba eneo la tukio kufanya tathimini ya uharibifu uliofanyika akiwa ameambatana na mkulima pamoja na mfugaji kisha yatafanyika makubaliano ya amani baina ya pande hizo mbili ili kila mmoja aweze kupata haki yake kisheria.