‘Sativa’ apatikana akiwa na majeraha

Dar es Salaam. Mkazi wa Mbezi wilayani Ubungo, Edgar Mwakabela (27) maarufu katika mtandao wa X (zamani Twitter) kwa jina la Sativa anayedaiwa kutoweka Juni 23, 2024 amepatikana mkoani Katavi, akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kwenye mitandao ya kijamii, Mwakabela amepatikana leo Alhamisi Juni 27, 2024 akiwa katika pori mkoani Katavi katika hali mbaya akiomba msaada wa kupelekwa hospitalini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amesema Mwakabela amepatikana leo Juni 27, 2024 asubuhi katika Hifadhi ya Katavi.

“Tulipata taarifa kutoka kwa watu kuwa wamekuta mtu mwenye majeraha hajiwezi yupo katika Hifadhi ya Katavi. Askari walifika eneo la tukio na kumhoji. Amesema alichukuliwa na watu wakaenda Arusha kutoka hapo walimpiga akapoteza fahamu na alivyozinduka akajikuta yupo msituni, akihangaika kujivuta hadi barabarani alipokutwa na wananchi,” amesema.

“Tunasubiri vipimo vya daktari kujua amepigwa na vitu gani lakini tumemkuta anachuruzika damu kichwani na miguu imevimba. Alipelekwa Kituo cha Afya Kibaoni, lakini kutokana na hali yake akahamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Tupindo,” amesema Kamanda Ngonyani.

Picha jongefu (video) iliyowekwa kwenye  mtandao wa X inamuonyesha Sativa akiwa porini mkoani Katavi akihojiwa na watu ambao hawaonekani katika video hiyo, akieleza kuumia kichwani, huku akivuja damu usoni.

“Naomba mnisaidie kichwa kinauma, wamenipiga sana miguu imevimba yote,” amesema Sativa akihojiwa kupitia video hiyo.

Taarifa zinaeleza Mwakabela ameshapelekwa Kituo cha Afya Kibaoni kwa ajili ya matibabu, jitihada zikiendelea kuratibiwa kumwezesha kupata usafiri wa ndege kutoka Mpanda hadi Dar es Salaam.

Katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu wameonyesha utayari wa kuchanga ikielezwa tiketi ya ndege imeshapatikana.

Taarifa zilizochapishwa  kwenye mtandaoni wa X, mtu aliyejitaja kuwa rafiki wa Mwakabela anaeleza Juni 23, alikwenda na kaka yake Ufukwe wa Coco na saa 11.00 jioni walirudi hadi Chuo cha Maji kwa usafiri wa bajaji waliyokodi kwa njia ya mtandao.

Baada ya kushuka eneo hilo walichukua usafiri mwingine hadi eneo la Utawala la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakatembea hadi lango la njiapanda ya kwenda Msewe na Changanyikeni.

Akiwa kwa kaka yake, saa moja usiku Mwakabela alipokea simu kutoka kwa rafiki yake iliyomtaka aende Kariakoo, inaelezwa alikubali wito na kumuaga ndugu yake kwamba anaelekea huko kisha atarudi Kimara anakoishi.

Inadaiwa saa 1:55 namba zake zote hazikupatikana, na walipojaribu kufuatili mwenendo wa simu zake ilioneka yupo katika Kituo cha Daladala cha Kibo.

“Ndugu wa Mwakabela iliwalazimu kurudi hadi lango la chuo kikuu kama unaelekea Msewe, kuwauliza bodaboda. Mmojawapo ambaye siyo anayeegesha katika kijiwe hicho, alisema uelekeo wa mtu wanayemtafuta haukuwa kama wa kwenda Kariakoo bali Kimara,” aliandika katika mtandao huo.

Katika hatua nyingine, Chama cha ACT-Wazalendo, kimekemea vikali tukio la kudaiwa kutekwa, kuteswa na kuumizwa Sativa, kikitaka hatua madhubuti zichukuliwe ili kukomesha vitendo hivyo.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Waziri kivuli wa Mambo ya Ndani wa ACT-Wazalendo, Dahlia Majid imeeleza kuwa Watanzania wameanza kuingiwa tena na hofu kukithiri kwa matukio ya wananchi kupotea, kuteswa kwa siku za hivi karibuni.

“Inasikitisha pia kuona vyombo husika havichukui hatua za haraka kwa wanaohusika na matukio hayo. Tunalaani kwa nguvu zote kuongezeka kwa matukio hayo bila hatua madhubuti kuchukuliwa.  

“ACT -Wazalendo tumechukua hatua za kumrejesha Dar es Salaam kwa ndege Sativa ili kupatiwa matibabu haraka na ya kibingwa, lakini tunataka hatua za haraka za uchunguzi zifanyike ili kubaini waliohusika na utekaji wa Mwakabela,” amesema Majid.

Related Posts