Bweni la Shule ya Wasichana Kaloleni laungua moto

Moshi. Bweni la Shule ya Wasichana ya Kiislam Kaloleni iliyopo Manispaa ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, limeungua moto na kuteketeza magodoro na vifaa mbalimbali vya wanafunzi.

Tukio hilo sio la kwanza kutokea shuleni hapo, Oktoba, 2020  moto uliteketeza vifaa mbalimbali vya wanafunzi vikiwamo vitanda na magodoro.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Februari 4, 2025, Kamanda Jeshi la zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema shule hiyo imekuwa na matukio mengi ya moto na kwamba wanachunguza chanzo cha tukio hilo.

Kamanda Mkomagi amesema matukio ya moto yaliyowahi kujitokeza kipindi kilichopita yanaviashiria vya hujuma kutokana na mazingira ya moto huo ulivyotokea.

“Majira ya saa 7:17 mchana leo Februari 4, 2025 tulipokea taarifa za tukio la moto katika shule hii ya Wasichana ya Kaloleni, kwa hiyo tulifika mara moja eneo la tukio na tulikuta jitihada mbalimbali za uokozi zikiendelea,” amesema Kamanda Mkomagi.

Amesema wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na wa awali unaonyesha moto huo haukusababishwa na hitilafu ya umeme.

“Inaonyesha hakuna uhusiano wowote wa moto na hitilafu ya umeme, kwa hiyo kuna vyanzo vingine tumeweza kuvibaini na tunaendelea kuvichunguza ili kujua chanzo hasa ni kitu gani,” amesema Kamanda Mkomagi.

“Hili tukio sio mara ya kwanza kutokea, miaka ya nyuma kulishatokea matukio matatu, tulikagua na tukawapa taarifa na mapendekezo ya nini cha kufanya na tulitoa elimu.

“Kujirudia kwa matukio ya moto katika shule hii, ndio kunatufanya tuingie katika uchunguzi wa kina kujua hasa nini kinasababisha matukio kujirudia katika shule hii.”

Akizungumza mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Sumaira Sajir amesema moto huo umetokea wakati wakitoka darasani kwenda kula chakula cha mchana na bado hawajui chanzo chake kwa kuwa ndani ya chumba hicho, vifaa vinavyotumia umeme ni taa peke yake.

“Ilikuwa muda wa kwenda kwenye chakula cha mchana umefika, tukasikia kelele za moto tulipokuja tukakuta moto unawaka kwenye chumba chetu, hatujajua chanzo ni nini maana kwenye hiki chumba kitu cha umeme tunachotumia ni taa peke yake,” amesema Sumaira Sajir.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Muhamed Migeto amesema vitu vilivyoathiriwa na moto huo ni vifaa vya wanafunzi vilivyokuwamo ndani yakiwamo mabegi na magodoro.

“Moto umeteketeza bweni na chumba namba tatu kimeathirika zaidi kwa kuungua mabegi ya watoto,” amesema Migeto.

Related Posts