Ferooz: Ahoua kaziba pengo la Chama

MSANII wa Bongo Fleva anayejulikana kwa jina la Ferooz ‘Bosi’ humwambii kitu kuhusu mshambuliaji wa Simba, Ahoua Jean Charles aliyekuwa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita na amemtabiria kuandika rekodi ya kibabe mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Ferooz amesema ni shabiki wa Simba damu na anavyocheza Ahoua  mwenye mabao saba ya Ligi Kuu hadi sasa, ana imani ni mmoja wa mastaa watakaoibuka vinara mwisho wa msimu.

“Kwa aina ya uchezaji wake, naona kaziba pengo la Clatous Chama ambaye kwa sasa yupo Yanga, maana kuondoka kwake kulituumiza, ila kaja kuondoa makovu na kutupa raha,” amesema Ferooz na kuongeza;

“Sina maana siwakubali wachezaji wengine Simba, ila kwa huyo jamaa ni zaidi, kwani akiwepo uwanjani unajua kuna kitu atakifanya cha faida kwa ajili ya timu.”

Msanii huyo ambaye aliwahi kutamba na wimbo wa Starehe aliyomshirikisha Professor Jay amesema, imani yake msimu huu ni Simba kunyakua ubingwa wa ligi kuu.

“Nauona ni msimu wa Simba kufanya vizuri kimataifa na ligi ya ndani, ina wachezaji wazuri, jambo la msingi watulie na wajitolee kwa ajili ya timu kila kitu kinawezekana,” alisema Ferooz.

Related Posts