Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2023, ina lengo la jumla la kuhakikisha Taifa linakuwa na mfumo wa elimu na mafunzo unaoweza kumuandaa Mtanzania mwenye maarifa, stadi na mtazamo chanya utakaomwezesha kuchangia katika kuleta maendeleo endelevu.
Malengo mahsusi ni pamoja na kuwa na mfumo, muundo na utaratibu nyumbufu wa kumwezesha kila Mtanzania kujiendeleza kwa njia mbalimbali kitaaluma na kitaalamu; kutoa fursa mbalimbali za elimu na mafunzo nchini; kuwa na elimu na mafunzo yenye viwango vya ubora unaotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa na kuwa na rasilimali ya kutosha na yenye umahiri na weledi stahiki kuendana na vipaumbelevya Taifa.
Mengine ni kuwa na usimamizi na uendeshaji madhubuti wa elimu na mafunzo nchini; kuwa na mfumo endelevu wa ugharimiaji wa elimu na mafunzo na kuwa na mfumo wa elimu na mafunzo unaozingatia masuala mtambuka, ikiwemo elimu ya afya ya mazingira, magonjwa na majanga, utafiti na maendeleo ya sekta ya elimu na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika utoaji wa elimu na mafunzo.
Elimu ya awali inalenga kumwandaa mtoto kimakuzi, kimwili, kiakili, kimaadili, kijamii na kijinsi na kumwezesha mtoto kujitambua mwenyewe na mazingira yanayomzunguka.
Pia ngazi hiyo ya elimu inalenga kubaini mtoto mwenye mahitaji maalumu na kumpa fursa stahiki; kumwezesha mtoto kumudu lugha mbalimbali na kumwandaa mtoto kujiunga na elimu ya msingi.
Elimu ya Msingi inakusudia kumwandaa mwanafunzi kuwa na stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu; kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuwasiliana kwa lugha fasaha, ikiwemo lugha ya Taifa ya Kiswahili, lugha za kigeni, lugha ya alama ya Tanzania, lugha ya alama mguso na breli na kumjengea mwanafunzi misingi ya uadilifu na kuheshimu utawala wa sheria.
Malengo mengine ni kumwezesha mwanafunzi kutambua, kuheshimu na kudumisha utamaduni wa Mtanzania na umoja wa kitaifa, na kutambua tamaduni nyingine; kumjengea mwanafunzi ubunifu, uwezo wa kudadisi, kufikiri kiyakinifu na kutatua matatizo; kukuza vipaji, vipawa, stadi za kazi, michezo na Sanaa na kumwezesha mwanafunzi kutambua na kutumia sayansi na Tehama katika kujifunza na kuendesha maisha ya kila siku.
Aidha, ngazi hiyo ya elimu pia inalenga kukuza maarifa, ujuzi na mwelekeo wa kutunza mazingira, kuheshimu usawa wa kijinsi, kumwezesha mwanafunzi kutambua masuala mtambuko na kumtayarisha mwanafunzi kuendelea na elimu ya sekondari.
Elimu ya sekondari inakusudia kupanua, kuimarisha, na kuendeleza maarifa, stadi, na mtazamo chanya uliopatikana katika ngazi ya elimu ya msingi; kumwezesha mwanafunzi kuelewa na kulinda misingi ya utamaduni (mila na desturi), umoja wa kitaifa, tunu za Taifa; na kuthamini haki za binadamu na wajibu unaoendana na haki hizo.
Pia, kujenga uelewa wa mwanafunzi kuhusu demokrasia, umuhimu na mipaka yake; kujenga utamaduni na umahiri kwa mwanafunzi katika kujisomea, kujiamini, kujiendeleza kwenye nyanja za sayansi na teknolojia, maarifa ya kinadharia,
kiufundi, kiujasiriamali na kupenda kufanya kazi na kumwezesha mwanafunzi kutumia stadi za lugha mbalimbali.
Malengo mengine ni kumwezesha mwanafunzi kutambua uwajibikaji wa pamoja wa kutunza afya, kuthamini usawa wa kijinsi na kusimamia utunzaji endelevu wa mazingira.
Aidha, sera inataja kuwa ngazi hii ya elimu inalenga kuimarisha misingi ya uadilifu na kuheshimu utawala wa sheria na kujenga ujuzi na stadi mbalimbali zitakazomwezesha mhitimu kujiunga na elimu ya juu na mafunzo ya amali sanifu baada ya elimu ya sekondari, kujiajiri, kuajiriwa, na kuyamudu maisha kwa kutumia mazingira yake.
Elimu ya juu inalenga kupanua, kuimarisha, na kuendeleza maarifa, stadi, na mtazamo chanya uliopatikana kabla ya kujiunga na elimu ya juu; kumwezesha mwanafunzi kupata maarifa na stadi za juu za kitaaluma na kitaalamu na kuandaa wanataaluma na wataalamu kwa ajili ya sekta mbalimbali.
Malengo mengine ni kuimarisha misingi ya uadilifu na kuheshimu utawala wa sheria na kujenga uwezo wa wanataaluma na taasisi za elimu ya juu katika kutoa na kuendeleza maarifa mapya kupitia utafiti, machapisho yenye ubora na kutatua changamoto za kijamii.