WAKATI Tanzania Prisons ikiendelea kujifua kwa ajili ya mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah amesema kikosi chake kipo tayari na Mashujaa wajiandae kisaikolojia kuacha pointi tatu.
Prisons inatarajia kushuka uwanjani Februari 6, kuikaribisha Mashujaa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya ukiwa ni wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo na mchezo wa kwanza kwa Kocha Josiah aliyerithi mikoba ya Mbwana Makata aliyesitishiwa mkataba kutokana na matokeo mabaya na sasa kazi inamsubiri kocha huyo.
Josiah alisema wamekuwa na muda mzuri wa kujiandaa na mechi za kirafiki walizocheza kwani zimeonyesha matumaini kwake ya kufanya vizuri na kujinasua nafasi za chini.
Alisema mechi dhidi ya Mashujaa wanahitaji ushindi ili kuongeza ari, morali na nguvu kikosini akieleza kuwa maandalizi waliyofanya lazima wapinzani hao waache alama tatu Sokoine.
“Tumekuwa na maandalizi mazuri, vijana wanajituma na kuonesha nia ya ushindi, tunataka kuanza kwa kishindo mzunguko wa pili tukiwakaribisha Mashujaa, hatutaki matokeo mengine” alisema Kocha huyo.
Kipa wa timu hiyo, Edward Mwakyusa alisema mazoezi waliyonayo ikiwamo mechi za kirafiki zinawapa morali na matumaini ya kuweza kubadili matokeo waliyonayo.
“Hatupo sehemu nzuri hivyo tunapoanza mzunguko wa pili hesabu ni kutafuta pointi tatu kila mechi, naamini kila mmoja kwa uwezo na juhudi binafsi tutafikia malengo” alisema Kipa huyo.
Championship vita nzito, ukipigwa umeachwa
PAMOJA na kushuka daraja msimu uliopita, Mtibwa Sugar na Geita Gold zimeonyesha nia ya kurejesha heshima yake kuisaka tena Ligi Kuu, huku Mbeya City na Stand United ‘Chama la Wana’ nazo zikiongeza presha.
Hadi sasa zimechezwa mechi 17 katika ligi ya Championship na vita imeonekana kuwa nzito katika hesabu za kupanda Ligi Kuu na kukwepa kushuka daraja.
Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu uliopita imeonyesha kasi kubwa ikivuna pointi 44, huku Geita Gold wakikusanya alama 36 na kung’ang’ania nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Mbeya City walioshuka daraja misimu miwili nyuma hawapo pabaya wakikaa nafasi ya tatu kwa alama 35 sawa na Chama la Wana walioikosa Ligi Kuu misimu mitano sasa.
TMA wanaoshiriki ligi hiyo kwa msimu wa pili wapo nafasi ya tano na pointi 31 sawa na Mbeya Kwanza walioshuka daraja misimu minne sasa wakiikosa Ligi Kuu.
Huko mkiani Biashara United iliyopokwa pointi 15 ndiyo inaburuza mkia kwa alama nne, huku Cosmopolitan ikiwa nafasi ya 15 kwa pointi tisa na Kiluvya ikifunga tatu za mwisho kwa alama 10 sawa Transit Camp.
Straika wa Mbeya City, Kilaza Mazoea amesema ushindani uliopo katika ligi hiyo ndiyo unaowapa nguvu na morali kupambania nafasi ya kurejea Ligi Kuu baada ya msimu uliopita kukwama.
Amesema kila mchezaji kikosini ndoto yake ni kuona anaandika heshima ya kupandisha timu hiyo Ligi Kuu na kila mechi kwao ni fainali ya pointi tatu.
“Ushindani ni mkali lakini hilo linatufanya kupambana kutafuta ushindi kila mechi, kiu na ndoto ya kila mchezaji ni kuona City inarejea Ligi Kuu, kila mechi kwetu kwa sasa ni fainali,” amesema nyota huyo mwenye mabao matano.