Simba bado haina uhakika wa kumtumia mshambuliaji wake Kibu Denis katika mechi inayofuata ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate, Alhamisi, Februari 6, 2025.
Mshambuliaji huyo aliumia katika kipindi cha pili cha mchezo uliopita wa Simba dhidi ya Tabora United ambao timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora na nafasi yake kuchukuliwa na Ladack Chasambi.
Akizungumza na Mwananchi leo Februari 4, 2025 Daktari wa Simba, Edwin Kagabi amesema kuwa mchezaji huyo anaendelea na matibabu na hadi sasa hakuna uhakika kama atacheza mechi hiyo japo anaendelea vizuri
“Mchezaji wetu alipata changamoto katika sehemu mbili kwenye mchezo wetu dhidi ya Tabora United. Alipata shida kwenye enka na pia kwenye sehemu ya robo tatu ya chini ya mguu. Kwa hivyo hali yake hadi sasa hivi iko vizuri na anaendelea na matibabu.
“Tuko katika hatua ya pili ya matibabu ni hamsini kwa hamsini uwezekano wa yeye kuwepo. Kwa hiyo kuna vitu tutaangalia leo na kesho kabla ya kuamua uwepo wake katika mchezo unaofuata wa Fountain Gate.
“Lakini kiujumla hali yake si mbaya sana hivyo nipende kuwatoa wasiwasi mashabiki na wapenzi wa Simba kwamba hali yake si mbaya sana,” alisema Kagabo.
Kibu amekuwa mchezaji tegemeo wa Simba katika ligi kuu na mashindano mengine ambapo mara kwa mara amekuwa akianza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 43.
Kuthibitisha hilo, mchezaji huyo ameanza katika kikosi cha kwanza cha Simba kwenye michezo saba kati ya 16 ya ligi ambayo timu yake imecheza, akiingia kutokea benchi katika mechi tano huku akikosa mechi nne tu kwa sababu ya kuuguza majeraha.
Akizungumzia hali za wachezaji wengine, Kagabo alisema tofauti na Kibu, wachezaji 23 waliobakia wako katika hali nzuri wakijiandaa na mchezo huo wa Alhamisi ambao timu hiyo inahitaji kushinda ili iendelee kuongoza msimamo wa ligi.
Simba imeweka kambi ya siku mbili jijini Dodoma ambapo Jumatano, Februari 5, 2025 itaondoka kwenda Babati ambako siku hiyohiyo itafanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ambako mechi dhidi ya Fountain Gate itachezwa Alhamisi, Februari 6, 2025 kuanzia saa 10:00 jioni.