Arusha. Kama sio kutoijua sheria vizuri, pengine Clara Kachewa angepata kifuta machozi cha Sh505 milioni alichokuwa akilidai Shirika la Umeme (Tanesco), baada ya kupigwa shoti ya umeme iliyosababishwa na waya wa umeme ulioangukia kwenye nyumba yao Tabata Dar es Salaam.
Ajali hiyo ya umeme imemsababishia Clara Kachewa madhara ya kudumu ya kupoteza kumbukumbu.
Kutokana na ajali hiyo na madhara hayo aliyoyapata, alifungua kesi ya madai dhidi ya Shirika la Umeme (Tanesco) kwa uzembe wa kushindwa kuondoa nyaya za umeme zilizoangukia kwake, licha ya kutoa taarifa mara kadhaa.
Katika kesi hiyo alikuwa akidai fidia ya Sh505 milioni, hata hivyo amekwama na hajaweza kuambulia chochote baada ya Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, kutupilia mbali kesi yake kutokana na kuchelewa kuifungua.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa Januari 30, 2025 na Jaji Hussein Mtembwa imesema kuwa kesi hiyo ilifunguliwa nje ya muda uliowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Ukomo kwa kesi za madai ya madhara.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, kesi za aina hiyo zinapaswa kufunguliwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
Mbele ya Jaji Mtembwa, mdai huyo akiwakilishwa mama yake, Lukresia Kachewa alikuwa akidai fidia ya Sh5milioni kwa ajili ya uharibifu maalumu na Sh500 milioni zikiwa ni uharibifu wa jumla wa uvunjaji wa wajibu wa huduma, riba yake kwa asilimia saba kuanzia tarehe ya hukumu hadi tarehe ya malipo kamili na gharama za kesi.
Clara alifungua kesi hiyo ya madai namba 24781 ya mwaka 2024, kupitia mama yake Lukresia Kachewa na mdaiwa wa kwanza alikuwa Tanesco wa pili Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Awali, Aprili 24, 2017 mdai na mama yake walikuwa wakiishi kwenye nyumba yao iliyopo Tabata Mtambani, Ilala jijini Dar es Salaam, ghafla nyaya za umeme zilizounganishwa na jirani yao ziliangukia kwenye nyumba yao.
Baada ya tukio hilo, mama mzazi wa mlalamikaji (Lukresia) alikimbilia katika ofisi za Tanesco, Tabata Liwiti na kuripoti tukio hilo ila Tanesco hawakuondoa nyaya hizo wala kukata umeme kutoka kwenye waya huo ulioanguka.
Ildaiwa kuwa, Septemba 16, 2017 Lukresia aliripoti tena kwa Tanesco kuhusu waya wa umeme ulioanguka kutoondolewa na hadi Oktoba 2018 Tanesco haikuwa ameondoa waya huo.
Ilielezwa kuwa, Lukresia alituma taarifa Tanesco na kupewa namba ya kumbukumbu ya kuripoti ILL 10/192018 TB 1198.
Novemba mosi 2018, waya wa umeme ulioanguka ulisababisha shoti ya umeme, hivyo kusababisha majeraha makubwa na ya kudumu kwa mlalamikaji.
Ilidaiwa kuwa, baada ya tukio hilo, huku akiwa hana fahamu, mdai alikimbizwa Zahanati ya Tabata ‘A’ kwa matibabu na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana kisha Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Juni 12, 2019, katika Hospitali ya Amana iliwasilisha fomu ya fidia iliyoonyesha hali ya jeraha na uchunguzi wa daktari ulieleza kuwa, mlalamikaji anaweza kupoteza kumbukumbu kutokana na uharibifu wa ubongo.
Aidha, taarifa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili ilieleza kuwa, mlalamikaji alipoteza fahamu kutokana na kuumia kwenye ubongo kutokana na shoti ya umeme.
Kwa upande wao wadaiwa walipinga madai hayo na kuwasilisha pingamizi la awali kwamba shauri hilo halitekelezeki, kwa kuwa limewasilishwa nje ya muda, kinyume na Kifungu cha 6 cha Sehemu ya Kwanza ya Jedwali la Sheria ya Ukomo (LLA), iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Mdai aliwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili Issa Chundo, huku wajibu maombi wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Grace Lupondo, pingamizi hilo la awali lilijadiliwa kwa njia ya maandishi.
Akiwasilisha hoja za pingamizi hilo, Wakili Grace aliipitisha Mahakama kwenye uamuzi wa Mahakama ya Rufani ili kuunga mkono hoja yake.
Alieleza kuwa, majeraha hayo ya kudumu kwa mdai yaliyotokana na shoti ya umeme iliyotokea Novemba mosi, 2018, mdai huyo alipaswa kuwasilisha malalamiko yake kabla ya Novemba 10, 2021.
Amesema kwa kuwa hilo halikufanyika kwa wakati unaofaa, mlalamikaji alifanikiwa kuomba kuongezewa muda na waziri anayehusika ila licha ya hatua hiyo, mdai huyo alipaswa kuwasilisha shauri Mei 9 2023 na siyo Septemba 2024.
Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa walioathiriwa (Law of Torts), mdai alipaswa kufungua madai hayo ndani ya kipindi cha miaka mitatu tangu tukio lilipotokea.
Baada ya kusikiliza hoja za pingamizi hilo la awali, Jaji Mtembwa, amekubaliana na hoja za upande wa washtakiwa akisema shauri hilo limefunguliwa baada ya kuisha kwa muda uliowekwa na sheria, kwa kuwa mdai alikubali na kukiri kwamba, shauri limeanzishwa baada ya kumalizika kwa muda uliowekwa na sheria.
Amesema Kifungu cha 44 (1) cha LLA kinampa mamlaka waziri kuongeza muda ila hawezi kuongeza muda hadi zaidi ya nusu ya kipindi kilichowekwa wazi kisheria.
Amesema kabla ya kuendelea, atachunguza kama kuongezwa kwa muda na waziri ni halali na kuwa mdai alipaswa kuwasilisha dai lake kabla ya Novemba 11, 2021 ila hilo halikufanyika.
“Ifahamike kwamba, kwa kuzingatia kifungu cha 44(2) cha (LLA), pale Waziri anapotoa muda wa nyongeza kuhusiana na shauri lolote, masharti ya sheria yatatumika kwa shauri hilo kana kwamba ni marejeo ya muda wa ukomo,” amesema.
Jaji huyo amesema waziri kuongeza muda ulipaswa kuanzia Juni 26, 2023 hadi Oktoba 9, 2024 na hakuwa na mamlaka ya kuongeza muda zaidi ya Mei 11, 2023 na kwa kuwa shauri hilo liliwasilishwa nje ya muda, ikiwa agizo la waziri la kuongeza muda lilikubaliwa kwa sababu ya msamaha.
“Kwa sababu muda wa awali uliowekwa na sheria, ambao ni miaka mitatu, uliisha Novemba 11, 2021, ninaona agizo la waziri likidai kuongeza muda kuanzia Juni 26, 2023 hadi Oktoba 9, 2024 na haufanyi kazi,hakuwa na mamlaka ya kuongeza muda zaidi ya Mei 11, 2023 ,” amesema.
Kuhusu ulemavu, Jaji Mtembwa amesema kifungu cha 15 cha LLA kinaeleza kuwa, utakuwa ni msamaha, ikiwa katika tarehe ambayo haki ya kuchukua hatua inaongezeka, mtu huyo hawezi kuanza kesi, kwa hiyo wakati huo utatengwa hadi tarehe ambayo ulemavu utakoma au wakati mtu anakufa.
“Kwa maneno mengine, wakati huanza baada ya tarehe ya ulemavu kukoma au juu ya kifo. Katika hali ambayo, hakuwezi kuwa na mashtaka kupitia mtu mwingine kama katika kesi ya papo hapo kwa sababu inachukuliwa kuwa ulemavu umekoma, mwakilishi wa kisheria atawasilisha kesi ikiwa mtu huyo atakufa,”amesema Jaji.
Jaji huyo amesema katika kesi hiyo, iliwasilishwa kupitia mtu mwingine kwa sababu mdai anakabiliwa na ulemavu kutokana na mshtuko wa umeme ulioharibu ubongo wake, hivyo, hawezi kujiendesha mwenyewe.
“Kwa kuzingatia uagizaji wa kifungu cha 3(1) cha LLA, shauri hili linatupiliwa mbali bila agizo lolote kuhusu gharama, kulingana na hayo hapo juu, nakubaliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba, shauri hili limewasilishwa nje ya muda uliowekwa,” amehitimisha Jaji.